Lydia mollel – Lindi. 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Rajab Telack amewataka wakazi wa Wilaya ya Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla, kuwa tayari kuwapokea Watalii wanaotembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara na kutumia fursa hiyo kufanya biashara za bidhaa za Utalii ili kuwaingizia kipato.

RC Telack ameyasema hayo wakati akiongea na Waandishi wa Habari ndani ya Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara wakati wa mapokezi ya Meli ya Saba kuingia Hifadhini humo katika kipindi cha mwezi Februari ikiwa na idadi ya watalii 120 kutoka Mataifa mbalimbali Duniani.

 

Amesema, mfululizo wa safari za Meli za Watalii ndani ya Hifadhi hiyo ni kiashiria kwamba filamu ya Tanzania The Royal Tour iliyochezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta matokeo chanya kwa Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa, Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA inatarajia kupokea Meli nyingine zaidi za watalii Mwezi March na April hivyo wakazi wa Mkoa huo watumie vyema ujio wa Meli hizo.

Aidha RC Telack pia ametumia fursa hiyo kuwaalika watu wote wenye bidhaa zinazopendwa na watalii na kuziuza wakati wa safari za wageni ndani ya Hifadhi hiyo huku  akisisitiza kuwa TAWA imejenga jengo la kisasa na maalumu kwa ajili ya wafanyabiasha wa bidhaa za kitalii, hivyo walitumie jengo hilo ipasavyo.

Awali, Mkuu wa Hifadhi hiyo, Mercy Mbogelah, alisema majengo ya kale yaliyojengwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita kama vile msikiti mkubwa na mkongwe kuliko yote katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki na ngome ya Mreno ni vivutio vikubwa vya watalii vinavyowafanya watalii wengi kumiminika katika Hifadhi hiyo.

Amesema, “lakini pia  kutokana na historia hiyo kubwa ndani ya Hifadhi ya Kilwa kisiwani  Mwaka 1981 Shirika la Kimataifa la UNESCO liliipa hadhi Hifadhi hiyo na kuwa Hifadhi ya Urithi wa utamaduni wa Dunia na baadae Mwaka 2023  kuwepa hadhi nyingine kuwa “Man and Biosphere Reserve”. Vigezo vyote hivi vimetajwa kuwa mojawapo ya sababu za watalii wengi kutoka nje kupenda kuitembelea.”

Hata hivyo, maboresho  ya miundombinu wezeshi ya utalii yaliyofanywa na Serikali kupitia TAWA nayo imetajwa kuwa miongoni mwa sababu za watalii wengi wa ndani na nje kupenda kutembelea na Kutalii ndani ya Hifadhi hiyo.

Naye Afisa Utalii wa Hifadhi hiyo, Shindawangoni Rajabu amesema Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara imekuwa ikipokea Meli kubwa za watalii na Mwaka huu wa 2024 imepokea Meli nyingi zikiwa na idadi kubwa ya watalii katika kipindi kifupi ikilinganishwa na miaka mingine yote na inatarajia kuendelea kupokea Meli nyingine zaidi za watalii kutoka Mataifa mbalimbali Duniani.

Hata hivyo ongezeko la idadi ya Meli zenye idadi kubwa ya watalii ni kiashiria tosha kuwa Hifadhi hiyo inaendelea kivutio kizuri zaidi Duniani.

Wataalam wabobezi China, Tanzania wajadili maboresho Kiuchumi
Umeme: Dkt. Biteko agusia uchorongaji Visima vya Jotoardhi