Kocha wa Simba SC amembadilishia majukumu kiungo wake kutoka nchini Mali Sadio Kanoute, na pia ameweka wazi kuwa hawana sababu yakushindwa kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Katika kuhakikisha wanafanikiwa kutengeneza na kutumia nafasi zinazopatikana katika mchezo wa kesho Jumamosi (Machi 02) dhidi ya Jwaneng Galaxy, Benchikha amemuandaa Kanoute kucheza nafasi ya Mshambuliaji Msaidizi akicheza nyuma ya Mshambuliaji wa kwanza kutoka kwenye nafasi yake ya Kiungo Mkabaji.

Kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ ambao Simba SC waliibuka na ushindi wa mabao 6-0, Kanoute alicheza kwenye nafasi hiyo ya nyuma ya Mshambuliaji na kufanikiwa kufunga ‘Hat Trick’.

“Alicheza vizuri sana kwenye nafasi ya mshambuliaji namba 10, anatumia vizuri mipira inayokosewa na mabeki wa upinzani, nadhani atatupa kitu kwenye mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy akicheza kwenye nafasi hiyo,” amesema Benchikha

Amesema mchezo wa kesho Jumamosi (Machi 02) ni muhimu zaidi kwao kushinda na ndio sababu ameandaa mbinu tofauti tofauti ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi na kutinga hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo ya Klabu Bingwa Barani Afrika.

“Hatuna sababu na hatutakuwa na sababu ya kutoa kama tutashindwa kufuzu, najua mpira una matokeo ya kushangaza lakini tumejiandaa vizuri, ni mchezo muhimu sana kwetu katika safari ya kuingia hatua ya Robo Fainali,” amesema Benchikha.

Mlinda Lango namba moja wa Simba SC, Aishi Manula akizungumzia mchezo huo wa kesho Jumamosi (Machi 02), amesema ni mchezo mgumu ambao ni lazima wapate ushindi kuweza kuweka hai malengo yao ya kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

“Ni mchezo wa kufa na kupona, ni mchezo ambao wanasimba wote wanauangalia kwa jicho la kufuzu, wachezaji tutapambana na Inshallah, tutapata ushindi, tunaomba mashabiki waje uwanjani kwa wingi kwa sababu uwepo wao utatuongezea hamasa zaidi sisi wachezaji kuweza kuimaliza mechi na kupata ushindi,” amesema Manula.

Simba SC inahitaji ushindi wowote kuweza kufuzu hatua ya robo fainali bila kuangalia matokeo ya Wydad Casablanca ya Morocco ambao wenyewe watacheza na Asec Mimosas kwenye mchezo mwingine wa Kundi hilo.

Matokeo yoyote nje ya ushindi yatatoa nafasi kwa Waarabu hao kutinga hatua ya Robo Fainali kama watawafunga Asec Mimosas.

Hiyo inatokana na timu hizo mbili (Simba SC na Wydad) kulingana pointi (zote zikiwa na pointi sita), lakini Simba SC ina faida ya matokeo mazuri baina ya timu hizo mbili ‘Head to Head’.

Aga Khan, TMJ wasitisha huduma za NHIF
Gamondi: Ni vita ya kuongoza Kundi D