Mabingwa wa Soka nchini Hispania FC Barcelona inafikiria kumsajili golikipa, David de Gea ambaye ni mchezaji huru, kwa mujibu wa ripoti.
De Gea amebakia bila klabu baada ya kuondoka Manchester United majira ya joto yaliyopita wakati mkataba wake ulipoisha.
Hapo awali alikuwa amekubali masharti ya mkataba mpya Old Trafford hadi klabu ilipoghairi ofa hiyo na kujaribu kumpa mkataba mpya kwa malipo ya chini, na Mhispania huyo hatimaye kuamua kuondoka baada ya miaka 12 ya kukaa klabuni hapo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 amebakia bila klabu na mechi yake ya mwisho ya ushindani ilikuwa United ilipofungwa 2-1 na wapinzani wao Manchester City kwenye fainali ya Kombe la FA Juni mwaka jana ambapo alikosolewa kwa kufungwa mabao yote mawili.
Lakini sasa gazeti la Katalunya la Mundo Deportivo limeripoti kwamba hivi karibuni anaweza kurejea kwenye soka akiwa na Barcelona.
La Blaugrana hao wamebakia na matatizo ya kifedha, walitumia euro milioni 3.4 pekee katika ada za uhamisho msimu uliopita wa joto, huku gharama yao ya msimu wa baridi ya euro milioni 40 ilitumika kumnunua Mshambuliaji wa Brazil, Victor Roque na wanaona kusajiliwa bila malipo kwa De Gea kama ni suluhu la gharama nafuu.
Mlinda mlango wa sasa Marc-Andre ter Stegen amekuwa akihusishwa na kuhamia Saudia katika wiki za hivi karibuni, huku Inaki Pena akicheza vizuri msimu huu na huenda akakabiliwa na nia ya kuhama.
Katika hatua hii, kuna uwezekano mkubwa kwamba De Gea atatumika mbadala wa Ter Stegen.
De Gea alikuwa kwenye mazungumzo juu ya kuhamia Real Madrid msimu uliopita wa joto baada ya Thibaut Courtois kupata jeraha, lakini wakachagua kumsajili Kepa Arrizabalaga kwa mkopo kutoka Chelsea.
Bayern Munich vile vile walikuwa kwenye soko la kutafuta Mlinda Lango msaidizi na walimfikiria De Gea kabla ya kumgeukia mchezaji wa kimataifa wa Israel, Daniel Peretz.
Klabu ya Nottingham Forest na Al Shabab inayoshiriki ligi kuu ya Saudi Arabia zote zilikuwa na nia ya kumsajili De Gea wakati wa dirisha dogo la usajili la Januari, lakini hatua hizo hazikutimia.