Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa amesema baada ya miaka miwili kushiriki michuano ya Baraza la soka Kusini mwa Afrika ‘COSAFA’ na kukosa ubingwa awamu hii wamejipanga kurudi na kombe.

Katika miaka miwili waliyoalikwa, mwaka wa kwanza walifika fainali na kutolewa na Msumbiji na mwaka jana walitolewa hatua ya Nusu Fainali na Senegal hivyo hii ni mara ya tatu watashiriki mashindano haya yatakayoanza Machi 17 hadi 25.

Akizungumzia maandalizi ya timu Dar es salaam, Kocha Pawasa amesema baada ya kufanya mazoezi ya kwenda na kurudi kwa zaidi ya wiki moja, leo Ijumaa (Machi Mosi) wataingia kambini rasmi kufanya maandalizi ya mwisho.

“Lengo letu msimu huu ni kwenda Afrika Kusini na kurudi na kombe, tunaendelea vizuri na maandalizi, wachezaji wako vizuri kwa mapambano,” amesema na kuongeza

“Kwa kipindi chote tulichoshiriki tumekuwa wanafunzi bora, kama Benchi la Ufundi tumeimarika, nayahimiza makampuni mbalimbali kujitokeza kuiunga mkono timu na sisi tunawaahidi mwaka huu tunakwenda kupeperusha vyema bendera ya Tanzania,” amesema

Mchezaji Sadiki Salum amesema kwa mazoezi wanayofanya anaamini watafanya vizuri kwani timu iko na morali ya hali ya juu.

Bayern Munich wanamtaka Andy Robertson
Kocha Jwaneng aipiga kijembe Simba SC