Polisi Mkoani Morogoro, ameingilia kati Sakata la Kikongwe wa miaka 119, Mkazi wa Kijiji cha Misegese kilichopo Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro, Bibi Stamili Kaloloma ambaye anadaiwa kutelekezwa na watoto wake watano, ambao hawamtunzi wala kumpatia mahitaji yake muhimu.
Hali hiyo, inatukia licha ya Watoto hao kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kupewa maagizo ya kumtunza kutokana na uzee wake, ambapo Polisi Kata wa Kata hiyo Mkaguzi Msaidizi, Michael Rasha kuona ipo namna ya kufamfanya kikongwe huyo apate msaada.
Mkaguzi Rasha amewaita watoto hao ambao wanaishi maeneo mbalimbali Nchini ikiwemo kwenye Majiji makubwa pamoja na kuwashirikisha Maafisa Ustawi wa Jamii, ili kuhakikisha Bibi huyo anapata matunzo pamoja na haki zake za msingi.
Amesema, ni lazima kila mmoja asimame kwenye nafasi yake kwani wazazi wana haki ya kupatiwa huduma zote muhimu kama ambavyo wao walijitoa kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji na kukua kwa afya hadi kufikia hatua ya kujitegemea.
“Kitendo cha kugomea kumtunza mzazi ni Ukatili lakini pia ni hatari kwa maisha ya mzazi maana kinaweza kupelekea kifo cha mapema,” alisema.
Kwa upande wao Majirani wa Kikongwe huyo wamesema wamekuwa wakijitahidi kumpa msaada, lakini pia kuwasiliana na watoto wa Bibi huyo bila kupata matumaini jambo ambalo liliwafanya wamtafute Polisi anayesimamia Kata hiyo, ili kuwatafuta kisheria.