Shirika linalojishughulisha na kuokoa maisha ya watoto wa shule, Amend Tanzania limewataka Madereva wa bodaboda katika jiji la Tanga kutokwepa mafunzo ya usalama barabarani na huduma ya kwanza yanayotolewa.

Afisa Programu wa shirika hilo, Ramadhan Nyanza ametoa wito huo wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Amend kwa waendesha Bodaboda kutoka Shakamai, Kata ya Magaoni Jijini Tanga.

Amesema, mafunzo hayo yanayotolewa chini ya Mradi wa usalama barabarani wa shirika hilo kwa ufadhili wa Serikali ya Uswisi kupitia Foundation Botnar, yanatolewa bila malipo kwa lengo la kuongeza uelewa wa sheria za barabarani na njia bora za madereva wa Bodaboda kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza.

Nyanza ameongeza kuwa, shirika hilo ambalo pia limejenga Miundombinu ya usalama barabarani katika maeno kadhaa wanazovuka watoto wa shule, linalenga kuwafikia waendesha Bodaboda 500 katika Jiji la Tanga.

“Tayari tumeshatoa mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva zaidi ya 250 wa bodaboda. Wengi wao wanahitaji mafunzo ili kuzuia ajali zisizo za lazima na kupunguza athari za ajali kupitia huduma ya kwanza,” alisema.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mwendesha Bodaboda, Hamis Shemnkai alimpongeza Amend kwa kuendesha mafunzo ya huduma ya kwanza alisema kuwa majeruhi wengi wa ajali wakiwemo madereva wa bodaboda walipoteza maisha kwa kukosa ujuzi wa huduma ya kwanza.

Dereva mwingine wa Bodaboda, Shaaban Rama alisema mafunzo hayo ni muhimu na yanatakiwa kuwa ya lazima kwa waendesha Bodaboda.

Watoto wamtelekeza Mzazi wao wa miaka 119
Mazoezi yazikutanisha Club tano Dodoma