Wizara ya Madini imevutia ushiriki wa Wanawake katika uvunaji wa rasilimali ya Madini muhimu ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uchumi wao na Pato la Taifa.
Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Jerry Slaa ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wanawake wanaoshiriki kwenye Sekta ya Uziduaji kama Sehemu ya maadhimisho ya wiki ya wanawake jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Wanawake wanaojishughulisha kwenye shughuli za Sekta ya Madini wamekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uchumi wao na Pato la Taifa.”
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Wanawake wanaweza kushiriki katika shughuli mbalimbali zilizomo katika mnyororo mzima wa thamani madini ikiwemo, utafiti, uchimbaji, uchakataji, uongezaji thamani, uuzaji wa madini na utoaji huduma katika sekta ya madini.
“Uchimbaji wa madini unahusisha shughuli nyingi sio lazima mwanamke akashiriki moja kwa moja kuchimba bali kufanya kazi zinazoenda sambamba na uchimbaji na kiweza kujikwamua kiuchumi katika jamii yetu.” Alisisitiza Waziri Mavunde
Amesema Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa STAMICO imeendelea kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele na kuwezeshwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za madini zikiwemo uchimbaji madini, utafitaji masoko, uongezaji thamani yakiwemo madini ya makaa ya mawe.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji (TAWOMA), Semeni Malale ameishukuru wizara ya madini kupitia STAMICO kwa kuweka sera zinazomwezesha mwanamke kuingia katika shughuli za uchimbaji.
Amesema kwa sasa Serikali imeweka sera zinazohasisha usimamizi mzuri wa rasilimali madini zinazomuwezesha mwanamke kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uchimbaji madini wanawake kusaidia jamii.
Aidha ametoa rai kwa serikali kuweka mpango wa kurudisha ruzuku kwa wachimbaji wadogo itakayojikita katika kulipia gharama za utafiti na uchorongaji moja kwa moja ili kuwasaidia kupata taarifa sahihi za Maeneo yao ya uchimbaji.
Hafla hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kiwemo, katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju, Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Mkuu wa Mkoa wa Iringa na viongozi mbalimbali wa Serikali.