Eva Godwin, Bahi – Dodoma.
Baadhi ya Wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi katika Bwawa la Sulungai lililopo Wilayani Bahi Mkoani Dodoma, wameiomba Serikali kuwaongezea muda wa miezi mitatu kuendelea kuvuna Samaki kufuatia sitisho lililotolewa la kuzuia shughuli za uvuvi ili Samaki waweze kuzaliana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wananchi hao akiwemo Mfanyabiashara wa Mgahawa katika eneo hilo, Emelda Fabian amesema Bwawa hilo ni chanzo cha mapato yao, hivyo likifungwa kwa kushtukizwa litawaweka katika kipindi kigumu wao na familia zao.
Amesema, “Sisi wateja wetu wakubwa ni hawa wavuvi sasa wanapofungiwa ghafla hivi na sisi tutaishije jamani, wengine wameondoka na pesa zetu tunazowadai na ni kutokana wamefunga ghafla bila hata taarifa.”
“Wengine tunamikopo tunatakiwa kurejesha kilasiku pesa na sisi tegemezi letu ni hawa wavuvi sasa mmewafungia sisi tutaenda wapi, tunaiomba serikali mliangalie hili, tuna mikopo tunatakiwa kulipa na hao Wavuvi wengine warudi watulipe pesa zetu,” amesema Emelda
Naye Mvuvi Sadala Abdallah amesema siku saba walizopewa na Serikali kuhama ni chache hivyo wanaziomba mamlaka husika kuwaongezea muda wa kuondoka katika eneo hilo kwa miezi hiyo mitatu.
Kwa upande wake Niclous Bikale ameitaka Serikali pia kuwapatia elimu juu ya namna bora ya kuvua Samani wanaopatikana katika Bwa hilo kwani Samaki wake ni wadogo.