Wakati Droo ya hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikitarajiwa kupangwa Jumanne ya wiki ijayo, Klabu ya Young Africans, inaomba ipangwe na Asec Mimosas ya Ivory Coast ambayo ni kinara wa Kundi B, lililokuwa likizijumuisha Wydad Casablanca ya Morocco, Jwaneng Galaxy ya Botswana na watani wao wa jadi Simba SC.

Katika kundi hilo, Simba SC imefuzu kwa kushika nafasi ya pili sawa na Young Africans ambayo ilikuwa Kundi C, iliyopita na vinara Al Ahly, huku CR Belouizdad ya Algeria na Medeama ya Ghana zikishindwa kupenya Robo Fainali.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe, ameweka wazi kuwa wanaomba Mungu wakutane Asec Mimosas ya lvory Coast katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Amesema kati ya timu tatu Petro de Luanda ya Angola, Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) na Asec Mimosas ambao mojawapo wanaweza kupangwa nayo, wao wanaitaka miamba hiyo ya lvory Coast.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Kamwe, amesema hata kama watapangwa na timu tofauti na Asec Mimosas, wanaamini wanaweza kufanya vizuri kutokana na ubora waliokuwa nao.

“Tuko tayari kukutana na yeyote katika hatua inayofuata, lakini ingetupendeza kakutana na Asec Mimosas ambao walionekana bora katika kundi lao, sisi Young Africans tunataka pia kuwaonyesha Simba SC kuwa hao ni wabovu kwa kumfunga na kuwaonyesha ubora wetu.

“Kwa tuliyopitia katika hatua ya makundi hatuna presha juu ya yeyote kati ya hao kwa sababu tumecheza na Al Ahly na CR Belouizdad ambao ni timu bora na Young Africans imefanikiwa kuingia Robo Fainali mbele ya Waalgeria,” amesema Kamwe.

Kuhusu kucheza Nusu au Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyotokea msimu uliopita kwenye Shirikisho, Kamwe amesema lazima ukweli usemwe kucheza fainali shirikisho ni tofauti na michuano waliyopo sasa.

“Mashabiki wa soka sio wajinga na kwamba hawajui mpira, hii michuano tuliopo sasa ni mingine, kumbuka imepita miaka 25 Young Africans haijacheza makundi Ligi ya Mabingwa ndiyo sasa, hivi leo uwaambie watu tutabeba ubingwa, hilo haliwezekani.”

“Hatuna historia nzuri katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa, sasa hivi tupo Robo Fainali hatuwezi kusema yaliyo mbele yetu kwa sababu hatujui tutakutana na nani licha ya kuwatamani Asec Mimosas,” amesema Kamwe.

Rais Samia ataka uzalendo usimamiaji Sekta ya Nishati
SJMT, SMZ watatua hoja 21 za Muungano