Wajumbe wa Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Menejimenti ya Mamlaka hiyo wameshiriki mafunzo ya siku tano ya Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST), wiki hii mjini Iringa baada ya kukamilika kwa moduli ya kupokea rufani za zabuni na malalamiko.

Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma Wizara ya Fedha, Dkt. Frederick Mwakibinga amesema Serikali inaendelea kujenga Mfumo wa NeST ambapo imeanza na moduli chache, lakini hadi sasa tayari kuna mafanikio mengi yameonekana kupitia moduli hizo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwazi, usawa na ushindani wa haki.

“Hivi sasa Serikali inaweza kupata taarifa za mwenendo wa zabuni moja kwa moja, inaweza kuona ni zabuni ngapi zimechakatwa, thamani yake, zabuni zilizotolewa hadi sasa na zipi zinaonekana zina matatizo ili hatua zichukuliwe. Mfumo uliopita haukuwa unaweza kufanya hilo,” amesema Dkt. Mwakibinga.

Aidha, Kamishna huyo wa Sera ya Ununuzi wa Umma ameeleza kuwa kukamilika kwa moduli ya kupokea rufani za zabuni na malalamiko kunaongeza ufanisi katika mnyororo wa ununuzi wa umma na ugavi kwakuwa itakuwa rahisi zaidi kutoa haki kwa uwazi.

“Hatua ya kukamilika kwa moduli ya kupokea malalamiko na rufani ni muhimu sana kwakuwa mambo yote sasa yatafanyika kwenye mtandao. Ninawapongeza sana kwakuwa hii moduli itasaidia kuongeza kasi ya kushughulikia malalamiko. Na kwakuwa kila kitu kinafanyika kwa uwazi ndani ya Mfumo huo mmoja, tunategemea hata hayo malalamiko nayo yatapungua,” Dkt. Mwakibinga aliongeza.

Alisema anafahamu kuwa ndani ya siku hizi tano, watapata nafasi ya kupitia kanuni za kupokea na kushughulikia malalamiko. Alitahadharisha kuwa ingawa kuna haki ya kulalamika na kukata rufaa, wapo baadhi ya wazabuni ambao wanakata rufaa kwa lengo la kuchelewesha michakato kwa makudusi huku wakifahamu kuwa wameshindwa kwa haki.

Alifafanua kuwa ingawa sheria na mahakama zimeweka uhuru wa kukata rufaa ni muhimu kuangalia uhuru huo usitumike vibaya kwa lengo la kukwamisha michakato na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi. Hivyo, aliwataka PPAA wanapopitia kanuni za rufaa kufikiria eneo hilo, “ninaamini, huko mbeleni mtu anayetumia uhuru wake vibaya kukwamisha michakato ya zabuni naye apate ujira wake,” amesema.

Akizungumza awali, Mwenyekiti wa Bodi ya PPAA, Jaji Mstaafu Sauda Mjasiri aliishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa Mfumo wa NeST ambao una moduli ya kupokea malalamiko na rufani za zabuni. Aidha, aliwapongeza wafanyakazi na wajumbe wa Bodi wa Mamlaka hiyo kwa jinsi wanavyohakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi kushughulikia malalamiko na rufani.

Rafael Leao azikataa Chelsea, PSG
Benchikha: Hatutaidharau Tanzania Prisons