Kiwango alichoonyesha Mshambuliaji Omary Marungu katika mechi iliyopita dhidi ya Singida FG, kimemkuna kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila akimpa maujanja mapya na katika michezo inayofuata kuisaidia timu hiyo.
Marungu alikuwa shujaa katika ushindi wa mabao 2-0 ugenini mbele ya Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita akichangia kwa kiasi kikubwa ushindi huo.
Marungu alihusika katika mabao yote mawili alipoingia kutokea benchi dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Seif Karihe.
Haraka katika dakika ya 69 akasababisha penalti alipoangushwa na kipa, Beno Kakolanya na katika dakika ya 75 akafunga bao la pili baada ya kuwachambua mabeki wa Singida na kuihakikishia alama tatu timu hiyo.
Kabla ya ushindi huo, Mtibwa Sugar ilikuwa imecheza mechi tatu mfululizo bila kuonja pointi tatu ikipoteza mbili dhidi ya Coastal Union 1-0 na Ihefu 3-2 na sare moja dhidi ya Dodoma Jiji na kubaki mkiani kwa pointi 12.
Katwila amesema Marungu ana kipaji kikubwa na ni mpambanaji ambaye anaweza kukupa chochote unapompa nafasi, akibebwa na kasi yake na kila kitu kinachohitajika kwa Mshambuliaji kufunga mabao.
Amesema Mshambuliaji huyo licha ya kutokuwa na uhakika wa namba kutokana na wazoefu waliopo kikosini akiwamo Charles Ilanfya na Seif Karihe lakini muda wake ukifika kila kitu kitakuwa sawa.
“Ni mchezaji mwenye uwezo japokuwa amekuta waliopo wenzake wana uzoefu, ila muda wake umefika na anaweza kufanya vizuri akiaminiwa, kimsingi naendelea kumuandaa kuweza kusaidia timu.”
“Kila mchezaji ana muda wake, nimeona uwezo na kipaji chake anaweza kuisaidia timu kwa kitu fulani na ukizingatia kwa sasa Ilanfya ana kazi tatu hivyo anaweza kuwa mbadala kwenye mechi zinazofuata,” amesema Katwila.
Kocha huyo amekiri kupitia wakati mgumu kwenye timu hiyo kwa matokeo yasiyoridhisha, huku akitoa matumaini kuwa kwa ushindi walioupata ugenini dhidi ya Singida Fountain Gate umeongeza kujiamini.