Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemsimamisha kazi Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Eng. Andrea Kasamwa kwa kushindwa kusimamia urejeshwaji wa miundombinu ya barabara na madaraja katika Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi na kupelekea barabara kuu zinanounganisha wilaya hiyo na maeneo mengine kufungwa.
Bashungwa amechukua hatua hiyo leo Machi 6, 2024 wakati akikagua mindombinu ya barabara katika Wilaya ya Liwale na kutoridhishwa na usimamizi wa kazi inayofanywa na Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Lindi.
Waziri Bashungwa akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Deo Ndejembi ameshuhudia urejeshwaji wa barabara ya Liwale – Nangurukuru iliyosombwa na maji ikisimamiwa na Mtaalam mwenye taaluma ya Falsafa kwa kusaidiwa na Wananchi wakati Mkandarasi akiwa hayupo eneo la Kazi.
Amesema, “haiwezekani sisi tutoke Dodoma hadi huku Liwale kutokana na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara iliyopo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelazimika kutoa Helikopta yake tufike huku, lakini hapa site hakuna Mkandarasi, mnaweka mtu aliyesoma falsafa kusimamia kazi ya ujenzi wa barabara.”
Aidha, Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta, kuleta Wataalam na kuhakikisha ndani ya siku nne barabara zote kuu na madaraja yanayounganisha Wilaya ya Liwale na maeneo mengine katika mkoa huo ambayo hayapitiki yawe yamefunguliwa na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Kadhalika, Waziri Bashungwa amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha ya kumtafuta Mkandarasi wa kujenga barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale km 175 kwa kiwango cha lami ili kumaliza changamoto inayoendelea kujitokeza ya kufungwa kwa barabara.
Bashungwa ameeleza kuwa Serikali itaanza kujenga kwa awamu barabara ya Nangurukuru – Liwale yenye urefu wa kilometa 230 kwa kiwango cha lami ambapo amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kutenga fedha na kumtafuta Mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi kipande cha kilometa 10 kwa kiwango cha lami.