Ili kuhakikisha inamaliza migogoro kwenye sekta ya michezo, Serikali imeunda mahakama ya usuluhishi na kuja na katiba ya mfano ambayo itafuatwa na vyama na mashirikisho yote nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro katika mkutano na viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo kujadili maendeleo ya michezo nchini.

Dk Ndumbaro amesema migogoro kwenye vyama vya michezo inarudisha nyuma maendeleo ya michezo ndio maana wametengeneza mfumo wa mahakama ya usuluhishi ili kuhakikisha migogoro ya michezo haiendi mahakamani.

“Ili kuhakikisha migogoro inakufa, tunakuja na katiba ya mfano ambayo itafuatwa na vyama vyote na tumeunda kamati ya watu 11 ambao wataisimamia na kushauri serikali na inaongozwa na Leonard Thadeo,” ameongeza

Pia amesema wameunda Kamati ya Mahusiano kati ya vyama na serikali ambayo itakuwa na wajumbe wanane na mwenyekiti wake ni Dk Yusuf Singo.

Amewataka viongozi wa vyama kuwa wazi katika fedha wanazopokea kwa kuzitolea taarifa ni nani kawapa kwa sababu duniani kuna tatizo la utakatishaji fedha na Tanzania ni moja ya nchi inayotajwa katika tuhuma hizo.

“Hatukupangii kiasi cha kutumia ila ukipata fedha utawajibika kutoa taarifa nani kakupa na lazima vyama muwe na ofisi na vyama vitakavyobainika kutokuwa na ofisi tutavifungia,” amesema.

Aidha, amesema kamati zilizoundwa zitakutana Dodoma Juni mwaka huu kutoa taarifa ya majukumu waliyopewa kutekeleza.

Dkt. Gwajima awafunda Wanawake wahitimu mafunzo ya uongozi GGML
Benchikha atimka Simba SC