Heri kwa Wanawake wote Duniani, ambao leo hii ijumaa ya Machi 8, 2024 wanasherehekea siku yao ya Kimataifa, ambayo pia hujulikana kama International Women Day – IWD, inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa – UN.
Rasmi siku hii iliasisiwa mwaka wa 1908, wakati wanawake 15,000 walipoandamana katika jiji la New York Nchini Marekani wakidai muda mfupi wa kazi, mishahara bora na haki ya kupiga kura, na kwa mwaka huu (2023), ikiwa na kaulimbiu isemayo, “Wekeza kwa Mwanamke, kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa Jamii.”
Taarifa kutoka Shirika la UN Women, inasema Dunia inahitaji ziada ya dola bilioni 360 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea kushughulikia usawa wa kijinsia chini ya Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs, huku siku ya Kimataifa ya Wanawake ikitambua mafanikio yao, bila kujali utaifa, ukabila, udini, utamaduni, lugha, hali ya kiuchumi au mwelekeo wa kisiasa..
Kihistoria, siku hii iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1911, huko Austria, Denmark, Ujerumani na Uswisi na kwa zaidi ya karne moja, dunia nzima imefanya Machi 8 kuwa siku maalumu kwa wanawake huku mwaka huu kitaalam ikisherehekewa kama siku ya 112 ya Kimataifa.
Wanawake watasherehekea siku hii, kwa kutafakari jinsi walivyopiga hatua kijamii, kisiasa, kiuchumi na kujadili changamoto wanazozipitia na jinsi ya kuzikabili na wazo la kuifanya siku hii kuwa ya kimataifa, lilitoka kwa Mwanaharakati wa kikomunisti, Clara Zetkin.
Watatafakari jinsi Ulimwengu ulivyopata maendeleo makubwa katika maeneo kadhaa, huku kukiwa hakuna nchi ambayo bado imepata usawa wa kijinsia kwani bado kuna mengi ya kufanyiwa kazi, ili kufikia lengo la maendeleo endelevu chini ya kifungu cha 5 cha ajenda ya 2030.
Tuukumbuke mwaka 1910 ambao Clara Zetkin alipendekeza wazo lake kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake Wanaofanya Kazi huko Copenhagen – Denmark, uliohudhuriwa na wanawake 100 kutoka nchi 17, na kulikubali pendekezo lake kwa kauli moja.
Kwa njia hii ya maadhimisho, wakati umefika wa kutafakari juu ya mafanikio yaliyopatikana, kuomba mabadiliko mapya na kusherehekea vitendo vya ujasiri na uamuzi wa Wanawake ambao wamejitofautisha katika historia.
Wanawake wanatakiwa kupewa nafasi sawa na Wanaume katika maeneo ya kazi na muda umefika kuona kuwa mwanamke si kiumbe dhaifu asiyejiweza, bali kutambua kuwa mwanamke ni mtu muhimu katika jamii na anapopewa nafasi, anaweza kufanya mambo makubwa yenye matokeo chanya.