Serikali Nchini, imevitaka vituo vyote vya Afya nchini kuanzisha kliniki maalum za kupima Magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Kisukari, Shinikizo la Juu la Damu (Presha) pamoja na kuwapima Selimundu (Sikoseli) watoto wanaozaliwa katika vituo hivyo.

Kauli hiyo, imetolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipofanya ziara katika Kituo cha Afya Chanika kwa lengo la kuangalia hali ya utoaji huduma ambapo ameridhishwa na huduma za Afya zinazotolewa katika kituo hicho kilichopo Jijini Dar Es Salaam.

Amesema, “sasa hivi tunataka kuona kila kituo cha Afya nchini kuwa na kliniki za magonjwa hayo hususan upimaji wa ugonjwa wa Kisukari, Shinikizo la Juu la Damu pamoja na Sikoseli.”

Ummy amesema, watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa Sikoseli wakianza kupata matibabu mapema inasaidia kuondoa fikra potofu kwa baadhi ya wazazi kuwa na imani za kishirikina kwa kudhani watoto wao wamerogwa kwa kuwa mtoto asipogundulika mapema huwa anaumwa mara kwa mara.

Ameongeza kuwa, miondombinu ya majengo itaongezwa katika Kituo hicho cha Afya Chanika ili iweze kupadishwa hadhi na kuwa Hospitali ya ngazi ya kwanza kwa kuwa kituo hicho kinafanya kazi kubwa ya kuwadumia wananchi wengi zaidi.

“Katika kituo hiki kwa siku wanatoa huduma za kuzalisha wanawake 30 hadi 50 kwa siku hali ambayo ukifananisha na baadhi ya Hospitali za Wilaya idadi hiyo ndio wanaozalishwa kwa mwezi, pia kituo hiki kwa mwezi kinaona wagonjwa kati ya 700 hadi 800, hii ni kazi kubwa na nzuri inayofanywa ma kituo hiki cha Chanika.” amesema Ummy

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji, Dkt. Zaituni Hamza ameishukuru Serikali na kuipongeza Wizara ya Afya chini ya Waziri Mhe. Ummy Mwalimu kwa kuendelea kuwatia moyo watumishi wa Afya kwa kuthamini kwa kile wanachokifanya hasa kutoa huduma bora kwa wateja.

Makala: Dunia inahitaji pesa kushughulikia usawa wa kijinsia
Siku ya Wanawake: Prof. Katundu agusia kasi kumtua Mama ndoo kichwani