Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Jamal Katundu leo Machi 8 2024 amewatakia Wanawake wote nchini kheri ya siku ya Wanawake duniani, na kusema kasi ya utekelezaji wa Miradi ya Maji ni chachu ya kumtua Mama ndoo kichwani.
Katika siku hii adhimu ya Machi 8 kila mwaka, Wanawake hutumia rangi za Zambarau, Kijani na Nyeupe ambazo kulingana na tovuti ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake inasema Zambarau inaashiria haki na heshima, Kijani matumaini na Nyeupe inawakilisha usafi.
Kaulimbiu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2024 ni “Wekeza kwa MwanaMke: kuharakisha maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”, ambayo inalenga uangaziaji wa umuhimu wa hatua za usawa wa kijinsia.
Siku hii pia hutoa fursa ya kuashiria maendeleo yaliyopatikana, na kuangazia ukosefu wa haki za Wanawake duniani kote, pamoja na madhara ya unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya Wanawake.