Watu tisa wamefariki katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Kiromo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani baada ya Basi dogo la abiria aina ya Coaster kugongana uso kwa uso na Lori.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva wa Lori kutaka kulipita gari jingine kwenye eneo lisiloruhusiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ametoa pole kwa majeruhi na wafiwa huku akiwataka Madereva kuwa makini na sheria za usalama Barabarani wawapo Safarini.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash amesema,  “waliofariki ni Wanaume saba, Wanawake wawili, Majeruhi ni Wanaume wawili na Mwanamke mmoja.”

Ajali hiyo, ilihusisha Lori aina ya Howo lenye namba za usajili T 503 DRP likivuta tela lenye namba za usajili T 733 DUQ, lililokuwa likitokea Bagamoyo Pwani kuelekea Dar es Salaam, kugongana na Toyota Coaster yenye namba usajili T 676 DSM, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Bagamoyo.

 

Wezi wa Maboya Kivuko cha Kigamboni waonywa
TANAPA kufanya ukarabati wa Barabara za Hifadhi