Kufuatia athari za Mvua za El-Nino ambazo zimeleta athari na uharibifu wa Barabara za Hifadhi, Mamlaka ya hifadhi za Taifa – TANAPA, inaandaa andiko la kitaalam litakalowasilishwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni – UNESCO, ili kufanya ukarabati wa Barabara hizo kwa kiwango cha zege na lami Serengeti.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya utalii na miundombinu, baada ya mvua kunyesha na kuleta uharibifu kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Amesema, njia ya kutumia andiko la kitaalam ndiyo iliyotumiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA), ambapo sasa imepata kibali cha kujenga barabara yenye tabaka gumu na kufafanua kuwa barabara hiyo ndiyo ndiyo inayoingia hifadhini Serengeti kwa  kuzingatia kuwa vivutio hivi viwili maarufu duniani vinapakana.

“Kuna barabara kuu nne zenye changamoto zaidi kutokana na upitaji wa magari makubwa ya abiria na mizigo yanayokwenda mikoa ya jirani ya Mara, Arusha, Manyara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu ambazo TANAPA ndizo inazozilenga katika mkakati wake wa mbinu mbadala ya tabaka gumu iwapo itakubalika,” amesema Matinyi.

Ameongza kuwa, kutokana na mvua hizo tayari TANAPA katika hatua za awali tayari imekamilisha matengenezo ya barabara  na sasa barabara hizo zinapitika na watalii wanaendelea kupata huduma  zinazostahili.

Serengeti ni Hifadhi ambayo inaliingizia Taifa fedha nyingi kwa kuwa watalii wengi hupenda kutembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kujionea wanyama wakubwa duniani na uhamaji wa wanyama aina ya nyumbu kwenda nchini Kenya na kwamba imechukua tuzo ya hifadhi bora Afrika kwa miaka mitano mfululizo.

Matinyi amesema, “Hifadhi hiyo imeingiza watalii 1,451,176 kwa miezi nane pekee kutoka ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Februari 2024 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo lengo lilikuwa ni kufikisha watalii 1,387,987 hivyo lengo hilo limevukwa kwa kipindi cha miezi nane tu.”

 

 

Ajali ya Coaster, Lori yauwa tisa Bagamoyo
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 11, 2024