Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssuouph Dabo, ameanza kuzinoa silaha zake kuhakikisha wanafanikiwa kupata ushindi katika mchezo wao unaofuata dhidi ya Young Africans.

Amesema anasahihisha makosa yao kwenye safu ya ulinzi na ushambuliaji ili kuwa makini katika mchezo ujao watakaocheza na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans.

Dabo amesema baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union, wamerejea katika uwanja wa mazoezi kwa ajili ya kusahihisha baadhi ya makosa yao.

Amesema sehemu zote zilikuwa na makosa, safu ya ulinzi na ushambuliaji, ameelekeza umakini wake katika maeneo hayo kwa sababu mechi inayofuata wanazitaka pointi tatu kwa kutowapa wapinzani nafasi ya kufanya mashambulizi.

“Washambuliaji nao wanatakiwa kuwa makini hasa nafasi tunazotengeneza, tunapoteza nafasi nyingi, katika hilo tunafanyia kazi kujiandaa na mchezo wetu unaofuata dhidi ya Young Africans, amesema kocha huyo.

Ameongeza kuwa, wanachoangalia zaidi ni kutafuta pointi katika kila mchezo uliopo mbele yao ili kufikia malengo yao pamoja na mashabiki kuona timu yao inacheza mpira mzuri na kupata matokeo mazuri.

Mwishoni mwa juma hili (Jumapili-Machi 17), Azam FC watakuwa nyumbani katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo ikiwakaribisha Young Africans, kwenye dimba la Azam Complex lililopo Chamazi jijini Dar es salaam.

GGML yatoboa siri kuongeza idadi ya Wanawake kwenye madini
Mohamed Salah afichua kuondoka Liverpool