Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis ameongoza zoezi la upokeaji na majadiliano ya matokeo utafiti wa awali wa hali ya biashara nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma, iliyotolewa leo na Meneja Uhusiano kwa Umma na Masoko Tantrade, Lucy Mbogoro imeeleza kuwa zoezi hilo limefanyika leo Machi 11, 2024 katika ukumbi wa Kilimanjaro sabasaba jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika zoezi hilo, Latifa amesema kuwa utafiti huo wa hali ya biashara nchini uliofanyika mwaka 2023 katika mikoa saba ya Tanzania bara na visiwani ulihusisha mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha na Unguja.
Ambapo amesema jumla ya kampuni 334 yaliyosajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) kwa yalifanyiwa utafiti huu.
Latifa ameongeza kuwa katika utafiti huo, sekta kumi zilihusika katika ukusanywaji wa takwimu hizo ni kilimo, uvuvi, madini, utalii, viwanda, ujenzi, huduma ya fedha na bima pamoja na biashara za jumla na rejareja.
Aidha amesema kuwa utafiti huu utaleta matokeo ambayo yatatumika kama fursa katika kuishauri serikali na wadau mbalimbali wa biashara.
Kwaupande mwingine Latifa amewapongeza wadau walioshiriki katika zoezi la ukasanyaji takwimu za utafiti huo wa awali, ambao ni Ofisi ya Takwimu (NBS), BRELA, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar(OCGS), Wakala wa Usajili Mtandao (Ega), Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti (ipsos Tanzania) pamoja na wakuu wa mikoa utafiti ulipofanyikia, huku pongezi za dhati zikienda Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Tantrade.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) Juma Khamis Juma alisema ni jambo zuri na la kupongeza kwa Tantrade kwani utafiti umefanyika na kutoa picha halisi ya biashara nchini Tanzania jinsi ilivyo.
Alisema Utafiti huo unaonyesha ni namna gani wataweza kujipanga kuanzia serikali kuu, Taasisi zake hadi kufikia kwa wananchi wanaohusika na masuala ya biashara.
”Ni jambo jema la kupongeza na kwa vile tumepewa takwimu halisi juu ya maoni ya wafanyabiashara tunaowahudumia kama serikali ,mapendekezo na changamoto walizotoa hapa sisi kama serikali tunaweza fanya kitu kwa masilahi mapana ya biashara na nchi kwa ujumla,”alisisitiza.
Naye Mdau wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI),Annah Kyango
alisema warsha hiyo ni muhimu kwao kwani imekuja muda muafaka kwasababu bila kufanya utafiti hawawezi kuendelea mbele.
Alisema bila utafiti serikali haitapata taarifa sahihi za kuweza kufanya maamuzi sahihi.”Warsha hii imekuja muda muafaka na ni muhimu kwa maendeleo ya taifa letu,”alisema.