Wakati kikosi cha Simba SC kikitarajia kuendeleza kasi yao ya ushindi kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kutoka kuichapa Coastal Union ya Tanga mabao 2-1 ugenini, wapinzani wao katika mchezo wa leo Jumanne (Machi 12), Singida Fountain Gate FC, wamesema utakuwa mchezo mgumu lakini “tunawafahamu ubora na udhaifu wao ulipo”.
Simba SC itaikaribisha Singida Fountain Gate FC katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam, saa 2:30 usiku, ambayo katika michezo sita iliyopita imeambulia sare moja mingine mitano ikichezea kichapo.
Katika mchezo huo, Simba SC watakuwa nyumbani Azam Complex baada ya Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kufungiwa kutokana na kutokidhi vigezo vya Bodi ya Ligi ‘TPLB’.
Timu hizo zote zinakutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara bila kuwa na makocha wake wakuu, Abdelhak Benchikha wa Simba SC akienda kuongeza ujuzi kwa kufanya kozi fupi na kuwaachia wasaidizi wake, Farid Zemiti na Selemani Matola, huku Singida Fountain Gate FC ikiwa imetimua benchi lote la ufundi na Ngawina Ngawina kupewa ukaimu wa kukiongoza kikosi cha timu hiyo.
Kuelekea mchezo huo Kocha Msaidizi wa Simba SC, Matola amesema maandalizi ya mechi ya leo dhidi Singida Fountain Gate FC yamekamilika na kwamba wanatambua siku zote hakuna mechi rahisi, lakini wamejipanga kulingana na ubora na madhaifu ya wapinzani wao.
Amesema itakuwa mechi ya ushindani kwani Singida Fountain Gate FC siku zote huwapa wakati mgumu, lakini wamejipanga kuhakikisha wanafanikiwa kuvuna pointi tatu katika mchezo huo wa leo.
“Tumechukuwa tahadhari kubwa katika safu yetu ya ulinzi kwa sababu tukifanya makosa katika nafasi hiyo kwa timu ya Singida Fountain Gate FC basi tunaweza kupoteza.
“Kulingana na ratiba tuliyokuwa nayo, tutakuwa na mabadiliko ya kikosi kwa kuwapa nafasi ya wachezaji wengine kupumzika na wale ambao hawakucheza mechi mbili zilizopita watapata nafasi,” amesema Matola huku akiwaita mashabiki kujitokeza uwanjani na kuahidi kuwafurahisha.
Kaimu Kocha wa Ihefu FC, Ngawina, amesema wamefanya maandalizi ya mwisho na wanaifahamu Simba SC hivyo wamejipanga kulingana na ubora wa wapinzani wao kuhakikisha wanaonyesha mchezo mzuri.
Ngawina amekiri katika michezo minne hawajapata matokeo mazuri, lakini wanaendelea walipoishia wenzake waliopita kuhakikisha wanamaliza dakika 90 kwa kutafuta alama muhimu.
“Tutacheza kwa tahadhari kubwa sana kwa sababu tunafahamu ubora wa Simba SC ikiwamo safu yake ya ushambuliaji, lakini pia kuna madhaifu yao katika ulinzi tukiwa makini tutawafurahisha mashabiki wetu,” amesema Ngawina.
Naye Nahodha na Mlinda Lango wa Singida Fountain Gate FC, Beno Kakolanya, amesema wanaifahamu Simba na wataenda kucheza mechi hiyo kwa tahadhari kubwa kwa kutafuta pointi ili kujiweka katika nafasi nzuri.
“Niliwahi kucheza Simba SC, hicho si kigezo kwetu kikubwa, ila nawafahamu wapinzani wetu na tutaingia kwa tahadhari kubwa ili kuweza kuvuna pointi tatu.” amesema Kakolanya.