Mshambuliaji kutoka nchini Senegal na Klabu ya Azam FC, Alassane Diao, atakuwa nje kwa muda wa miezi saba hadi tisa baada ya kufanyiwa upasuaji.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa Azam FC mwanzoni mwa msimu huu, amefanyia upasuaji wa goti ‘ACL’ jana Jumatano (Machi 13) Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Azam FC, Diao amefanyiwa upasuaji huo katika Hospitali ya Vincent Palloti, jijini Cape Town, Afrika Kusini.
Kwa mantiki hiyo Diao hatakuwa sehemu ya kikosi cha Azam FC msimu huu na sehemu ya msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa, kwa ajili ya kuuguza majeraha yake hayo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Medicover Hospitals, Majeraha ya ACL (Anterior Cruciate Ligament) mara nyingi hutokea wakati goti linapigwa kwa ghafla au mabadiliko katika mwelekeo, na kusababisha ligament kunyoosha au kupasuka. Wanariadha wanaojishughulisha na michezo kama vile soka, mpira wa vikapu, kandanda na kuteleza huathiriwa hasa na machozi ya ACL kutokana na miondoko ya kasi inayohusika.