Kocha Mkuu wa Tabora United, Goran Kopunovic amesema matokeo mabaya inayoyapata timi yake kwenye mechi za Ligi Kuu yanatokana na matatizo lukuki yanayoikabili timu hiyo.
Kocha huyo amesema baadhi ya viongozi wa timu hiyo wameshindwa kutimiza majukumu yao, kitu ambacho kimechangia kushusha ari ya upambanaji ya wachezaji.
“Tabora tuna kikosi bora chenye ushindani, lakini baadhi ya watu ndani ya timu wanawavunja moyo wachezaji na kusababisha mwenendo huu wa kusuasua, kitu ambacho siyo kizuri hata kwangu kama kocha,” amesema Goran Kopunovic
Kocha huyo raia wa Serbia amesema Ligi Kuu zote duniani ni kazi zinazohitaji umakini na zinaongoza kwa presha lakini hilo halipo kwao, jambo linalofanya hata wachezaji kushindwa kujituma na wanacheza mechi ya ligi kama wapo kwenye uwanja wa mazoezi.
Amesema hali kama hiyo inamfanya agomee ofa aliyopewa na Rais wa timu hiyo Salum Kitumbo ya kuongeza mkataba wa kuifundisha timu hiyo kwani kinachoendelea haoni kama kitakuwa na faida kwake wala timu kwa ujumla.
Tabora ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo ikikusanya pointi 21 katika idadi kama hiyo ya mechi ilizocheza msimu huu ambao ndio wa kwanza kwao tangu wapande daraja.