Kocha wa FC Porto, Sergio Conceicao amemshutumu Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kwa kuitukana familia yake wakati Waingereza hao juzi Jumanne (Machi 12) usiku wakishinda kwa mikwaju ya Penati dhidi ya timu hiyo ya Ureno na kujikatia tiketi ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2010.

Alipotakiwa kufafanua kilichotokea, Conceicao kupitia mkalimani wa Shirikisho la Soka Barani Ulaya ‘UEFA’ alinukuliwa akisema, “Wakati wa mchezo na kuelekea benchi yeye, kwa Kihispania, sijui ndio ilivyo kwa makocha wa Hispania, aliitukana familia yangu.

“Na kisha mwishoni, nilisema tafadhali usimtukane mtu ambaye hayupo hapa kati yetu, unapaswa kuzingatia mafunzo ya timu yako,” alisema Conceicao.

Hata hivyo, vyanzo vya Arsenal viliambia ESPN kwamba Arteta alikanusha vikali shutuma hizo.

Washika Bunduki walitinga hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa Penati 4-2 baada ya bao la Leandro Trossard dakika ya 41 kusawazisha mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 kwa uwiano wa bao 1-1 na kulazimisha mchezo kwenda muda wa ziada na baadae changamoto ya mikwaju ya Penati.

Wendell na Galeno mikwaju yao ya Penati iliokolewa na David Raya, lakini makocha hao wawili waligombana tena wakati wa kipenga cha mwisho.

Baada ya mechi, Arsenal na Arteta walikuwa na nia ya kuangazia usiku wa kihistoria ambapo hatimaye walimaliza msururu wa vipigo saba mfululizo katika hatua hiyo ya mashindano haya.

“Kwa timu kufanya hivyo wakati haijaweza kufanya hivyo kwa miaka 14, nawaambia ni nguvu,” alisema Arteta.

“Mpaka ni mdogo sana, unatafuta njia ya kufanya tena. Naona wanataka kiasi gani, wanajaribu kiasi gani na wanaweza kujitolea chochote kushinda. Ukicheza hivi mwisho mambo mazuri yanaenda vizuri.

“Sasa nitakaa nyumbani, nitaangalia timu nyingine tunazopaswa kucheza na kuanza mlima mwingine mkubwa wa kupanda.”

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Conceicao kugombana na kocha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Alimshutumu kocha wa wakati huo wa Chelsea, Thomas Tuchel kwa kumtusi wakati The Blues walipoitoa Porto katika hatua ya robo fainali Aprili 2021.

Conceicao pia alitoa madai kama hayo kuhusu kocha wa Manchester City, Pep Guardiola kufuatia mchezo wa hatua ya makundi kwenye Uwanja wa Etihad Oktoba 2020.

Arsenal wameungana na Real Madrid, Manchester City, FC Barcelona, Bayern Munich, Atlético Madrid, Borussia Dortmund na Paris Saint-Germain kwenye chungu cha droo ya robo fainali kesho ljumaa, huku washindi wawili waliobaki walitarajiwa kupatikana jana wakati Borussia Dortmund ilipotarajiwa kucheza dhidi ya PSV Eindhoven na Inter Milna dhidi ya Atletico Madrid.

Kopunovic afichua kinachoikwamisha Tabora Utd
Al Ahly wamrudisha fasta Benchikha