Mwekezaji na Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji, anatarajiwa kuwa sehemu ya wafanya uamuzi ndani ya klabu hiyo ikiwa pamoja na kusimamia usajili wa wachezaji kuelekea msimu ujao wa mashindano, imefahamika.

Habari za ndani ya klabu hiyo zinasema inatarajia kuandaa muundo mpya ambapo Dewji atakuwa sehemu ya watoa uamuzi wa mambo mbalimbali ikiwa pamoja na usajili wa wachezaji watakaoidhinishwa na benchi la ufundi.

Taarifa zinasema hali hiyo inakuja kufuatia kile kilichoelezwa klabu hiyo imekuwa haifanyi vizuri kwenye madirisha ya usajili kwa siku za karibuni.

Imeelezwa uongozi umekuwa ukileta wachezaji wengi ambao hawakidhi viwango vya kuichezea klabu hiyo kitu ambacho hata mwenyewe (Dewji) amekuwa akikilalamikia.

Taarifa zinaenda mbali zaidi na kusema Simba SC imekuwa haifanyi vizuri kwenye usajili tangu Dewji alipoondoka katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, imekuwa ikisuasua katika masuala ya usajili kiasi cha kutegemea wachezaji wale wale wa zamani huku idadi kubwa ya wageni wakionekana kuwa na uwezo wa kawaida.

“Hivi sasa klabu inaandaa muundo mpya kuelekea msimu ujao, Dewji atahusika kwa karibu zaidi na timu kuliko hapo awali, yaani atawekwa karibu zaidi katika mambo yanayoihusu klabu.

“Sasa atakuwa sehemu ya uamuzi utakaokuwa unachukuliwa kwenye klabu ikiwa ni pamoja na kufuatilia usajili wa wachezaji wapya, hii ina maana atakuwa anafuatilia kila kitu kinachofanyika au kutokea, kwa sababu ya haya yanayotokea.”

“Timu haifanyi vizuri, misimu mitatu sasa sawa na madirisha sita ya usajili, wachezaji wanaoletwa wako chini ya kiwango cha kuichezea klabu kubwa kama hii, hivi sasa kuna kelele za mashabiki wa Simba SC nchi nzima, watu hawaendi viwanjani, haya yote yamesababisha haya mabadiliko, lengo ni kuirudisha Simba SC ile ambayo watu wameizoea,” kimesema chanzo hicho.

Katika hatua nyingine, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC amesema kwa sasa akili yao wameielekeza kusaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao na si kingine.

Amesema mambo yote ya klabu, ikiwemo usajili yatajulikana baada ya msimu kumalizika.

“Nadhani kwa sasa Wanasimba tunapaswa tushirikiane ili tumalize ligi salama na kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao.”

“Baada ya hapo tutakwenda kukaa chini sisi kama viongozi wa Simba SC na kuangalia nini tufanye, wapi turekebishe, lakini kwa kuwa timu yetu msimu huu haijafanya vizuri, maana yake tuna wajibu wa kufanya maboresho makubwa ili tuwe na msimu ujao mzuri.”

“Kama jahazi linayumba, kuna mambo mawili, kwanza kupunguza mizigo ili likae sawa, au ugeuze, urudi pwani ili ujipange upya, kwa hiyo sisi kuna mambo tutayafanya ili kujiweka vizuri, sisi kama viongozi tunajua nini cha kufanya kuelekea msimu ujao,” amesema Ahmed

TAWA: Ukivamiwa na Mamba mtoboe macho atakuachia
Ajali za Barabarani: Madereva wa Serikali watajwa