Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba akijulikana kama Papa Wemba (R.I.P) na Antoine Christophe Agbepa Mumba maarufu kama Koffi Olomide walikuwa na ushindani mkubwa ulioleta upinzani mkali wa kimuziki katika historia ya muziki wa Kongo.

Wengi wakataka kujua ni nini hasa kilipelekea hali hiyo kati ya wakongwe hao wawili wa zamani kiasi ikapelekea Papa Wemba kumkakataza Koffi asihudhurie mazishi yake endapo atafariki, kitu ambacho kilitekelezwa na Koffi kama Wemba alivyotaka.

Ipo hivi, historia ya marafiki hawa wawili ambao walikuja kuwa mahasimu ilianzia mwaka 1970, wakati Koffi bado kijana ambaye alianza kuwa mshirika katika kundi la Viva La Musica kundi ambalo lilikuwa chini ya Papa Wemba.

Koffi Olomide (Kushoto) na Papa Wemba.

Mzee Papa Wemba hakuwa na hiyana, kwani alimpa jukwaa na kumuacha huru Koffi ili aweze kutimiza ndoto yake ya muziki na ndipo akampa ‘AKA’ ya kisanii akimuita ‘Olomide’ na hapo kazi ikafanywa hadi ilipofika mwaka 1986 Koffi alipoanza kufanya kazi peke yake kama Mwanamuziki wa kujitegemea na kundi lake la Quartiel Latin.

Chanzo cha tatizo:

Inasemekana kuwa shida ilianza mwaka 1993/1994, kutokana na kutokea kwa msuguano kati yao baada ya Mzee Papa Wemba kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na dansa kipenzi cha Koffi Olomide, Rosette Kamono kitu ambacho hakupendezwa nacho na kupelekea kisasi kwa Koffi kupoka mmoja Mabibi wa Wemba ili kupoza maumivu.

Watoto wa Malweka pale Kinshasa wanasema ngoma ikawa droo, lakini mtafaruku wa maisha (bifu) ukawa umeundwa rasmi na ilipofika miaka ya 1994/1996, sura nyingine ya mzozo kwa Koffi Olomide iliibuka baada ya kuhitilafiana na rafiki yake wa karibu Félix Nlandu ‘Wazekwa’ maarumu kama Mokua Bongo.

Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba ‘Papa Wemba’ (R.I.P).

Felix alikuwa ameanza kama mtunzi mahiri na rafiki wa Koffi Olomide hata kumsaidia katika utunzi wa baadhi ya nyimbo latika albam ya NOBLESS OBLIGE, lakini mwaka 1994 alianza kufanya kazi kwa Papa Wemba naye akijitafuta hapo akishiriki katika albamu za Wemba za FORIDOLE 1994 na POLE POSITION 1996.

Albamu hizi mbili zilimrudisha Papa Wemba kileleni baada ya kuwa ameshuka kiwango, kitu ambacho hakikumpendeza Koffi Olomide hata kidogo na hivyo kumuweka Felix Wazekwa katika hadhi sawa na Papa Wemba akidai ni msaliti na hawezi tena kuwa karibu yake, akisahau kwamba umaarufu wake, kughani kwake katika nyimbo, vyote vilisimamiwa na Wazekwa.

Upatanisho:

Hata hivyo, ilipofika mwaka 1996 kupitia marafiki zao wa karibu waliwaweka chini ili kumaliza tofauti zao (Papa Wemba na Koffi Olomide) ndipo wakatoa Albamu ya upatanisho wakiipa jina la WAKE UP, lakini mara baada ya hapo, uhusiano huo ulikoma na ‘bifu’ likaendelea kama awali hakuna aliyekubali kujishusha.

Antoine Christophe Agbepa Mumba, ‘Koffi Olomide’.

Papa Wemba alikuwa akimtuhumu Koffi Olomide kwa kukataa kugawana kwa usawa kiasi kikubwa cha fedha kilicholipwa na wafadhili wa mradi huo wa Albamu ya pamoja iliyorekodiwa katika Studio za Guillaume Tell, ambayo waliwashirikisha pia Wanamuziki kadhaa akiwemo mpiga gita mahiri na Kiongozi wa Wenge Musica BCBG wakati huo, Allan ‘Prince’ Makaba na baadaye kuanzisha mchakato wa kumshitaki Kofii Mahakamani akitaka alipwe chake, ili maisha yaendelee.

Wengine walioshirikishwa katika albam hii walikuwa ni Ballou Canta, Myriam Betty, Sylvie Ayoun, Yves Ndjock, Sungu Déba Félicien, Danos David Laurent (Nyboma Mwandido), Victor Philippe Guez, Bibi Den’s Tshibayi, Jean-Marie Motingia, Komba Mafwala Bellow, Miguel Yamba, Caien Madoka, Maika Munan Kashal Hilaire, Xavier Jouvelet na Beniko Zangilu (Popolipo).

Kuongezeka kwa uhasama.

Mwaka wa 1999 ulikuja na mambo mawili kwani Papa Wemba alikuwa kwenye kiwango cha juu na kundi lake la Nouvelle Ecriture, wakati Koffi Olomide alikuwa anatia huruma baada ya kupoteza karibu Wanamuziki wake wote muhimu waliomkimbia na kwenda kuanzisha kundi jingine la Quartiel Latin Academia.

Hili lilileta uhasama mkubwa na majibizano makali kwenye vyombo vya habari, kwani Papa Wemba alikuwa akikejeli masaibu ya Koffi kwa njia mbalimbali ikiwemo kwenye wimbo wa ‘Mzee Fula ngenge’ akisema ”Lofunde y’a mwana ntaba, ka se ati mokolo na moto wa koni, akimaanisha (kiburi cha mtoto wa mbuzi kinaisha wakati anapokanyaga kuni inayowaka moto).

Mwelekeo mwingine wa mzozo huo ulikuwa ‘Vita vya Wenge’. Wakati Papa Wemba alimuunga mkono waziwazi Jean Bedel au JB M’piana na kundi lake la Wenge BCBG, huku Koffi Olomide na King Kester Emeneya wakimuunga mkono Noel Ngiama Makanda ‘Werrason’ na kundi lake la Wenge Musica Maison mere, ambapo ukali wa vita yao hiyo ulienea hadi kwenye kizazi cha Wenge.

Vyombo vya Habari vinakuza mgogoro:

Vita hivi vya wakongwe, vilichezeshwa pia kwenye vyombo vya Habari, kwani watangazaji na waongoza shughuli katika matamasha mbalimbali walitia chumvi mijadala, huku wakiuza CD na DVD za kubadilishana zenye vijembe na hizi zilikuwa zinauzwa zaidi ya DVD ya muziki na watu kama akina Zacharie Bababaswe, walituhumiwa kuchochea uhasama.

Félix Nlandu Wazekwa, Mokua ‘Bongou’.

Juhudi za upatanisho zagonga mwamba:

Mara ya mwisho Koffi na Papa wapolishiriki jukwaa moja ilikuwa 2009, kwenye kuchangisha fedha katika klabu ya moja ya soka ambapo watu wakidhani wamepatana kumbe ilikuwa ni geresha kwani kuhusika wa upatanisho alidhani amefaulu lakini haikuiwa hivyo kwani moto ulikuwa bado ukifukuta kwa chini na hivyo suala hilo kushindikana.

Kifo kinawatenganisha:

Papa kwa upande mwingine alikuwa na uhusiano mbaya na kila rafiki wa karibu wa Koffi kama vile Verkys Kiamuangana aliyekuwa Afisa Mkuu wa SOCODA (chombo kinachoshughulikia haki za Wanamuziki na Watunzi) na hata waziri wa utamaduni wa wakati huo, Banza Mukalay pia hakuwa karibu naye akimtuhumu kwa ukaribu na hasimu wake.

Kwa kutumia njia hiyo, Koffi Olomide alimrushia ‘madongo’ Papa Wemba ili kukata kiu yake ya unangaji. Hata hivyo, Watu wanachoamini ni kwamba mzozo na migogoro wakati mwingine ni mizuri kwa kazi ya Wanamuziki ili kuleta ushindani wa tungo na hamasa, lakini sijui kama Papa Wemba na Koffi Olomide walifanya hivyo, kwani hawakuwahi kupatana hadi pale Papa Wemba alipolala kwenye nyumba yake ya milele mwaka 2016.

Kocha Dodoma Jiji anaitaka Ligi Kuu
Mrithi wa Lomalisa akaribia Young Africans