Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans ipo katika hatua za mwisho kumsainisha Beki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na klabu ya Saint Eloi Lupopo Chadrack Boka.

Taarifa zinaeleza kuwa Young Africans inakaribia kuipata saini ya mchezaji huyo anayecheza nafasi ya beki wa kushoto, ili kuchukua nafasi ya Joyce Lomalisa ambaye huenda akaondoka mwishoni mwa msimu, lakini ikiwa ni pendekezo la kocha Gamondi.

Mtoa taarifa kutoka Young Africans amesema kuwa Rais wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es salaam Hersi Said, yupo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa ajili ya kusaka baadhi ya wachezaji wa kuimarisha kikosi kuelekea msimu ujao 2024/25.

Imeelezwa kuwa Hersi pia amekutana na Rais wa Klabu ya TP Mazembe, Moise Katumbi kwa lengo la kuzungumza na kujadilia mambo mbalimbali ikiwamo uendeshaji wa timu, lakini na suala zima la Usajili wa wachezaji.

“Siyo huyo tu, kocha ametoa mapendekezo ya wachezaji kadhaa na suala la Mshambuliaji ndiyo limezingatiwa zaidi maana tangu alipoondoka Mayele (Fiston), hajapatikana mtu sahihi, waliokuja bado hawajaweza kukidhi mahitaji ya safu hiyo, pia tunaendelea kuimarisha safu ya ulinzi,” amesema mtoa habari huyo.

Young Africans ipo katika mipango ya kuachana na baadhi ya nyota wake, ambapo mbali na Lomalisa, yupo Mahlatse Makudubela maarufu kama ‘Skudu’ na Bakari Mwamnyeto ambaye hataongezewa mkataba, taarifa zikisema wakala wake amemtafutia timu nchini Afrika Kusini.

Habari zinasema kumekuwa na mvutano kati ya Augustine Okrah na Kennedy Musonda nani anatakiwa kuachwa kwa ajili ya kupisha usajili wa mchezaji mwingine ili kukiimarisha kikosi hicho.

BURUDANI: Kifo kilitenganisha 'bifu' la Papa Wemba, Koffi Olomide
Ibenge kuikacha Al Hilal, atajwa Simba SC