Hakika Afrika imejaaliwa kuwa na utamaduni wake wa asili ambao wakati mwingine unaweza kutafakari jinsi waasisi wake walivyopambania, ili kupata upekee kama si uhalisia na kujitofautisha.

Katika hili kuna mgawanyiko mkubwa wa kiimani, mtindo wa maisha na hata mapambo kama kupiga chale au kujichanja maeneo mbalimbali mwilini nk.

Wengine walienda mbali zaidi kutafuta upekee kwa kutoga masikio, kuweka ndonya, kutoboa pua, kuchanja chale na hata kung’oa jino moja ili wawe na mwanya, ingawa katika hili niliwahi sikia kwamba baadhi iliwalazimu kutokana na maradhi mfano kuumwa kichwa.

Walioumwa kichwa sana, inaaminika walichanja chale ili kupaka dawa kwani wakati ule hakukuwa na Hospitali au Zahanati, hivyo walipopata tiba hizo mbadala walipona na alama zilibaki wengine wakadhani ni urembo nao wakaiga.

Inasimuliwa kuwa, kuna wakati ulikuja ugonjwa ambao mtu alikuwa akiuma meno na kushindwa kula, hivyo walimng’oa jino moja ili pindi atakapofunga mdomo kwa maradhi, basi sehemu ya jino iliyotolewa ingetumika kupitishia chakula hasa uji.

Hata hivyo, miongoni mwa makabila ya Afrika ni alama muhimu ya tamaduni zetu walizojiwekea kwa kutumia vifaa vyenye ncha kali kama vile mawe, kisu na chupa kujichora maumbo au alama zenye kubeba maana, ujumbe fulani au urembo.

Urembo huu wa kudumu pia ulibeba taarifa kuhusu jamii fulani, kwa mfano kusini mwa Tanzania wanafanya tamaduni hii kabila la wamakonde na ukiwaona tu utajua huyu ni ‘Njomba’ huyu.

Kaskazini mwa Tanzania wapo Wamasai, wao huchanja sura zao kwa ustadi kutafuta urembo, nadhani ndio maana Wahenga walisema “ukitaka uzuri, sharti udhuruke” kama ambavyo pia watu wa Taifa la Ethiopia au Papua New Guinea wanavyoweka alama za chale kwenye miili yao.

Alama hizo zinaweza kubeba taarifa kuhusu cheo, hadhi katika jamii, ukoo, familia, ukubwa wa madaraka, hata pia kuonesha mtu anayehama rika, mfano picha hapo juu inaonesha mtoto wa kabila Nuer la nchi ya Kush (Sudani ya Kusini), alama za usoni mwake huitwa ‘gaar’ ambazo ni ishara ya kuvuka utoto kwenda utu uzima.

Bila shaka kuna mengi unayafahamu kutoka katika kabila lako, nianze na mimi huko kwetu kwa Mama yangu ugogoni Dodoma wanaweka ndonya, hiyo hukaa kwenye paji la uso kwa Wanaume isipokuwa Wanawake ambao wao huweka pande tatu kwenye paji la uso na pembeni mwa jicho la kushoto na kulia.

Ni urembo tu hakuna maana yoyote ya ziada, japo wakubwa wanasimulia kuwa ililazimu kufanya hivyo kwa wale waliokiwa wakiumwa kichwa na hiyo ilikuwa tiba ambayo baadaye ikaja kuwa mapambo, hivyo kazi ikawa ni kubwa kwani kila mtu alihitaji.

Ila sasa, uwekaji wake unatisha na hata kuumiza kwani Wataalam wa kuweka ndonya walichukua kikonyo cha Tunda la Mbuyu kisha kukichoma moto na kumuwekea usoni muhitaji au mgonjwa ili kufanikisha lengo.

Hakika Afrika ni sehemu pekee ya utamaduni asili wenye kustaajabisha, lakini wala siku hizi hatuutilii maanani tukihisi ndiyo maendeleo, HIVI NI NANI ALIYETUROGA. Je? unaifahamu alama yoyote ya utambuzi kulingana na matabaka ya asili ndani ya kabila lako? hii ni Dar24 Media karibu kwa maoni au kuongeza data za historia kuhusiana na mada hii.

Aziz Ki kusaini miwili Young Africans
Mgunda: Mechi ya Azam FC ni Fainali