Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, Umoja wa wanawake wanaofanya kazi katika Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML Ladies) wametoa darasa kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Kalangalala mkoa wa Geita ili kuwawezesha wanafunzi hao kujitambua.
Wanawake hao kupitia program waliyoipa jina la ‘Mentorship’, wamelenga kujenga ukaribu na wanafunzi hao kwa kuwapatia maarifa, ujuzi na uzoefu katika kazi wanazofanya kwenye mgodi huo na sekta ya madini kwa ujumla.
Akizungumza na wanafunzi hao wa shule Kalangalala wiki iliyopita mkoani Geita, Kiongozi wa msafara huo unaotembelea shule hizo za serikali, Hadija Kisatu alisema mwaka 2021 umoja huo ulipata wazo la kuanzisha program hiyo kisha kuanza kutekelezwa mwaka 2023.
Alisema programu hiyo ilianzishwa baada ya kuona kampuni nyingi za madini zinakosa wataalam wa kuajiriwa na migodi kutoka Geita, ukanda huo wa ziwa na shule za sekondari.
“Ni kutokana na uelewa mdogo wa kazi ambazo mathalani GGML inafanya, lakini pia masomo gani watoto wasome na kugundua kipawa chake. Hivyo tukaona kuna umuhimu wa kutembelea wanafunzi ili kuwajengea uwezo wa kuchagua masomo ya kusoma,” alisema.
Mjiolojia kutoka GGML, Janeth Luponelo naye alisema program huadhimishwa ili kuenenda na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo hufanyika Machi 8 kila mwaka.
“Mwanamke yeyote ni mama kwa sababu pia tunazaa watoto wa kike na wa kiume na wote tunataka wawe na ushindani sawa. Hivyo lazima kuhimiza kufanya vizuri darasani kwa usawa,” alisema.
Mbali na kuwaelezea wanafunzi hao kazi na idara mbalimbali zinazofanyika ndani ya mgodi huo, pia Luponelo aliwaeleza wanafunzi hao kwamba kuanzia sasa kila mmoja anatkiwa kuusikiliza moyo wake kuwa anataka kuwa nani.
Naye Ofisa Mwandamizi wa masuala ya mafunzo kutoka Idara ya Rasilimali watu, Lina Sitta aliwaeleza wanafunzi hao faida za program hiyo ya mentorship kwamba itawasaidia kujitambua, kujua madhaifu yao na uimara wao.
Makamu Rais Mwandamizi wa AngloGold Ashanti-GGML – Kitengo cha Ubisa/ Ushirika Afrika, Terry Stron alisema malengo ya kampuni hiyo ni kuwekeza kwa vizazi vijavyo kwani kuwekeza kwa wanafunzi hao ni sawa na kuwekeza kwa jamii ya Geita ijayo kwani watoto hao wa kike na kiume watakuja kuwa viongozi wa baadae.
Makamu Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia na ushirika Afrika, Simon Shayo alisema, “Programu hiyo ya GGML ladies inadhihirisha malengo ya kampuni hiyo katika kudumisha usawa wa kijinsia kwa maendeleo ya jamii. Tunajivuni kuunga mkono mpango huu ambao unaleta hamasa kwa wasichana wadogo,” alisema.
Mmoja wa wanufaika wa programu hiyo ni Adam Jonas, mwanafunzi wa kidato cha tano Kalangalala Secondary ambaye alisema programu hiyo imempatia ufumbuzi wa maswali mbalimbali aliyokuwa akijiuliza kutokana na mchepuo wa HGL anaousoma kwamba ataweza kuwa mjiolojia.
“Nimetambua mbali na jiolojia pia unaweza kusomea sheria na ualimu. Suala la msingi naomba GGML waendelee na programu hii katika shule mbalimbali ili wanafunze watambue fursa zilizopo mbele yao.
Naye Jasmin Jacob, mwanafunzi wa kidato cha tatu mchepuo wa biashara kutoka Kalangalala sekondari alisema programu hiyo imemuongezea uelewa wa namna ya kutimiza ndoto zake.
“Walezi wetu wametuelezea maisha halisi baada ya masomo. Wametupatia ujasiri wa kupambana kufikia malengo. Wametuelezea kazi mbalimbali zinazohusiana na mchepuo huo kwa mfano uhasibu, uhandisi na jiolojia,” alisema.