Lydia Mollel – Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa ametoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu suala la ujenzi usiokubalika katika soko la Chifu Kingalau, Mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Nsemwa, amesema kuna maeneo ya wazi katika soko hilo ambayo hayafai kwa ujenzi wowote.

Amesema, “kwenye soko hili kuna maeneo ya wazi ambayo yapo restricted ayatakiwi  kujengwa kitu chochote lakini kwa masikitiko makubwa tumepata taarifa kwamba muheshimiwa Diwani wa Kata ya Mwembesongo na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji katika katika Halmashauri yetu ya Manispaa Ally Rashid Kalungwana yeye amekiuka utaratibu na kuja kujenga vibanda eneo hili la wazi.”

Nsemwa ameeleza kwamba, Diwani huyo alipewa agizo la kubomoa vibanda hivyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama hadi tarehe 13 Machi, lakini hadi wakati huo hakuwa amekamilisha jukumu hilo, ambapo kufuatia hali hiyo, Kamati imechukua hatua ya kusimamia ubomoaji wa vibanda hivyo.

Aidha, amesisitiza kwamba Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wanaovunja sheria za ujenzi. Amewataka wote waliojenga katika maeneo ya wazi kubomoa mali zao wenyewe kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya, Ernest Komba amesema walipokea taarifa kuhusu ujenzi huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Soko, kufanya ufuatiliaji na kumsimamisha aliyekuwa anaendeleza ujenzi huo.

Hata hivyo, mtuhumiwa alikaidi amri hiyo na kuendelea na ujenzi, hivyo wakalazimika kutoa taarifa kwa mamlaka husika, ili kupata msaada zaidi.

Mwenyekiti wa soko, Khalid Mkungegele, amesema walitoa taarifa mara mbili kwa Mkurugenzi wa Manispaa na kuwatoa wale waliokuwa wanaendeleza ujenzi haramu lakini baadaye walirudi tena na kujaribu kujenga na sasa Kamati ya Ulinzi na Usalama imevunja vibanda hivyo.

Akizungumza kwa njia ya Simu Diwani wa Kata ya Mwembesongo na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Ally Rashid Kalungwana, amejitetea akisema hahusiki na ujenzi wa vibanda hivyo wala umiliki wake hivyo akisema maswali zaidi yaulizwe kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro.

Rais Mnangagwa: Wanaozalisha Almasi waongeze thamani
Wanawake GGML wawauma sikio Wanafunzi Kalangalala Sekondari