Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amehimiza Mataifa yanayozalisha Almasi Barani Afrika kuhakikisha wanaongeza thamani madini hayo ndani ya bara hilo ili kuepuka kuuza na kusafirisha Almasi ghafi nje ya nchi.
Alitoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Nchi Zinazozalisha Almasi Afrika (ADPA), uliofanyika mjini Victoria Falls, Zimbabwe katika hafla iliyohudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Constantino Chiwenga.
Alisema, lengo la kuanzisha ADPA ni kutafuta njia za ushirikiano katika kuongeza thamani ya madini hayo na pia kushiriki katika Soko la Kimataifa la Almasi kwa kulinda maslahi ya pamoja kwa kuwa kuuza Almasi ghafi ni sawa na kuuza ajira za wazawa kwenda kwa mataifa ya kigeni
Aidha, Rais Mnangagwa alizihimiza Nchi za Afrika kufikiria namna ya kununua Almasi zitakazoongezewa thamani ndani ya bara hilo badala ya kusubiri nchi kutoka nje ya Afrika kuwa wateja na wanunuzi wakubwa wa Almasi iliyoongezewa thamani.
Aliongeza kuwa, ni aibu kwa Nchi za Afrika zinalozalisha zaidi ya asilimia 60 ya Almasi ghafi duniani kushindwa kuongeza thamani madini hayo na kutaka changamoto hiyo iwe chachu ya kujenga Viwanda vya kuongeza thamani Madini ya Almasi pamoja na Madini ya Vito vingine.
Aidha, Rais Mnangagwa alisisitiza umuhimu wa Mataifa ya Afrika kuchukua udhibiti wa rasilimali zao za madini na kuzitumia kikamilifu kwa manufaa ya kiuchumi na maendeleo ya bara zima.
Kutoka upande wa Tanzania, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo aliongoza ujumbe wa Tanzania na kumwakilisha Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa ADPA.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mbibo aliushukuru na kuupongeza Uongozi wa ADPA chini ya Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Zimbabwe, Soda Zhemu kwa kuruhusu Lugha ya Kiswahili kutumika katika Mkutano huo kwa mara ya kwanza na kufungua njia kwa lugha hiyo kutumika katika Mikutano ya ADPA miaka ijayo.
Mkutano huo wa ADPA ulifanyika kwa siku tatu kuanzia Machi 12, 2024 na kuhitimishwa na Baraza la Mawaziri wa Umoja huo ambalo lilifanyika Machi 14, 2024.