Kocha Mkuu wa Atletico Madrid, Diego Simeone amesema alishindwa kudhibiti hisia zake kiasi cha kushindwa kushuhudia mikwaju ya Penati kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Inter Milan Jumatano ambao timu yake iliingia Robo Fainali ya mashindano hayo.
Mchezaji Federico Dimarco aliifungia Inter bao la kuongoza na kufanya matokeo kuwa 2-0 kwa michezo yote miwili kabla ya dakika mbili baadae Antoine Griezmann kusawazisha na dakika ya 87, Memphis Depay aliyeingia kipindi cha pili kufunga bao la pili na kufanya mchezo huo kwenda muda wa nyongeza.
Penati iliyopigwa na Mshambuliaji Lautaro Martinez wa Inter ilipaa juu ya lango, ikiwa ni baada ya kipa wa Atletico, Jan Oblak kuokoa matuta ya Alexis Sanchez na Davy Klaassen na kuivusha timu hiyo ya La Liga kwenye Robo Fainali.
“Sikuangalia wakati Penati zinapigwa,” alisema Simeone alipoulizwa kuhusu mikwaju hiyo ya Penati.
“Sio vizuri kwa mimi kuangalia, niliamua kutoangalia. Jan anastahili pongezi. Mara nyingi inakuwa ngumu kwetu kwenye hatua ya Penati.”
Atletico iliwahi kupoteza mchezo wa Fainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya wapinzani wao Real Madrid kwa mikwaju ya Penati mwaka 2016 katika jiji la Milan.
“Nilikuwa naangalia picha za mashabiki kwenye luninga, ni hisia kali,” alisema Simeone.
“Wakati timu ikiwa kama ilivyokuwa leo (juzi), matumaini yanaongezeka na kutengeneza shauku. Sisi ni moja ya timu nane bora Ulaya kwa mara nyingine tena, hiyo inaeleza mengi kuhusu timu yetu.”
Simeone aliipongeza Inter iliyofika Fainali za michuano hiyo msimu uliopita kuwa ni moja ya timu bora Barani Ulaya kwa sasa.
“Ni timu nzuri. Wanacheza vizuri, wana kasi, wana maamuzi, washambuliaji wao wanajituma sana. (Mabeki Stefan) Savic, Mario (Hermoso), Axel (Witsel) walikuwa na mchezo mzuri. Walicheza vile walivyotakiwa kucheza.” alisema Simeone