Kocha Mkuu wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Julien Chevalier amefunguka alichokuwa akikihofia wakati wa kupangwa wa Droo ya Michezo ya Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mwanzoni mwa juma hili.
Kocha Chevalier amesema hakutaka wala kutamani kupangwa na Young Africans katika hatua hiyo, huku akiwatabiria mabingwa hao wa Tanzania Bara kwenda Nusu Fainali mbele ya Mamelodi Sundowns.
Asec ilioongoza Kundi B, lililokuwa pia na Simba SC imepangwa kukutana na Esperance ya Tunisia katika mechi hizo za Robo Fainali zitakazopigwa mwishoni mwa mwezi huu, jambo lililoelezwa na kocha Chevalier kuwa ni ahueni kwa timu hiyo, tofauti na kama ingepangwa na Young Africans aliyoitaja kama moja ya timu aliyokuwa akiiogopa kukutana nao.
Kocha huyo, amesema kati ya vitu ambavyo alikuwa anahofia wakati inachezeshwa Droo ya mechi hizo za Robo Fainali pale jijini Cairo, Misri ilikuwa ni kupangwa na Young Africans aliodai ipo vizuri sana ndani ya misimu miwili mfululizo.
Amesema licha ya Young Africans kupangiwa mpinzani mgumu mwenye ubora mkubwa Afrika, Mamelodi Sundowns lakini kama ikijipanga vyema hasa kwa mchezo wa kwanza utakaopigwa jijini Dar es salaam inaweza kufanya kitu cha kushtua katika soka la Afrika kama ailivyofanya msimu uliopita ilipofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika bila kutarajiwa.
“Nilifurahi kuona sijapangwa na Young Africans, ndani ya kikosi cha wababe hao wa Tanzania kuna wachezaji niliowafundisha msimu uliopita akiwemo Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki na Yao Kouassi, nafahamu uwezo wao,” amesema kocha huyo Mfaransa na kuongeza:
“Ukiondoa hilo msimu uliopita Young Africans ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ingekuwa timu mbaya isingefikia hatua hiyo, naamini Young Africans ina nafasi ya kutinga Nusu Fainali licha ya kupangiwa Mamelodi Sundowns, inayoonekana kuwa tishio.”
Kocha Chevalier amefafanua zaidi kwa kusema; “Young Africans inacheza kwa ubora mkubwa iwe nyumbani au ugenini, wakati Asec kwa sasa imebomoka safu ya ushambuliaji, hivyo kama tungekutana nao safari yetu ingekuwa fupi mno.”
Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba ya mechi za Nusu Fainali, Mshindi wa mchezo kati ya Young Africans na Mamelodi atavaana na yule wa pambano la Asec Mimosas dhidi ya Esperance, hivyo kama zote zitavuka basi hatakuwa na ujanja wa kukiepuka kikombe kutegemana na matokeo ya kila mmoja kwenye mechi hizo za Robo Fainali.
Akiizungumzia Esperance aliyopangwa nayo, amesema amejipanga vizuri kupambana nayo na anaiona nafuu kubwa ya kupata matokeo kutokana na kiwango cha kikosi chake.
“Timu za Afrika Kaskazini zina nafuu kwa kuwa una nafasi ya kutengeneza ushindi mkubwa ukiwa nyumbani kwa kuwa ugenini huwa wanakuja kucheza kwa asilimia 50-60,” amesema kocha huyo
Licha ya Chevalier kuitabiria Young Africans kwenda Nusu Fainali na kuchekelea kutokutana nayo kwenye hatua hiyo ya Robo Fainali, lakini ukweli ni kwamba Young Africans inaonekana kuwa na kibarua kizito mbele ya Mamelodi inayoshikilia taji ya Ligi ya Afrika (African Football League) kutokana na rekodi za wababe hao wa Afrika Kusini kutisha kwa sasa.
Timu hizo zitakutana kwa mara ya pili baada ya awali kucheza mechi za Raundi ya Pili katika msimu wa 2001 na Young Africans kufungwa 3-2 ugenini kabla ya kutoka sare ya 3-3 nyumbani, na safari hii Vijana wa Miguel Gamondi wataanza kuwa kuikaribisha Mamalodi Kwa Mkapa kati ya Machi 29-30 kisha kurudiana nao Afrika Kusini Aprili 5-6.