Vinara wa Ligi Kuu ya Soka nchini England ‘Arsenal’ wamepangwa kukutana na Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich katika mchezo wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ‘UEFA Champions League’
UEFA wamepanga Droo ya hatua hiyo leo Ijumaa (Machi 15) majira ya mchana mjini Nyon nchini Uswiz, na miamba hiyo inakwenda kukutana kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010.
Ni dhahir Mshambuliaji wa FC Bayern Munich Harry Kane atarejea nyumbani kwao London, England kwa mara ya kwanza, baada ya kuondoka mwanzoni mwa msimu huu akitokea Tottenham.
Akiwa Spurs Kane alikuwa na bahati ya kuifunga Arsenal walipokutana nayo katika michezo ya Ligi Kuu ya England, na sasa itamlazimu kuonesha uwezo wake wa kufanya hivyo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.
Wakati Arsenal wakipangwa dhidi ya FC Bayern Munich, Mabingwa watetezi wa Michuano hiyo ya Barani Ulaya Manchester City watamenyana na Real Madrid, huku Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain wakipewa FC Barcelona ya Hispania.
Atletico Madrid ya Hispania imepangwa kupepetana na miamba ya soka kutoka nchini Ujerumani Borussia Dortmund.
Michezo ya Nusu Fainali inaonyesha Mshindi wa mchezo kati ya Atletico Madrid/Borussia Dortmund atakutana na mshindi wa mchezo kati ya Paris Saint-Germain/FC Barcelona.
Nusu Fainali ya pili itashuhudia Mshindi wa mchezo kati ya Arsenal/Bayern Munich akipambana na Mshindi kati ya Real Madrid/Manchester City.
Ikumbukwe kuwa Mchezo wa Fainali wa Michuano hiyo kwa msimu huu 2023/24, umepangwa kuchezwa jijini London katika Uwanja wa Wembley mnamo Juni Mosi.