Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya Kijamii kwamba Imam wa Msikiti wa Nyankumbu ambaye pia ni Mwalimu wa Madrassa, Abdulrahman Yassin ametekwa na watu wasiojulikana, bali walikamatwa na wenzake kwa tuhuma za kihalifu.
Akizungumza na Vyombo vya Habari, Kamanda Jongo amesema Imam huyo anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kiuhalifu na si vinginevyo.
Amesema, “kutokana na aina ya tuhuma alizonazo, kulikuwa na watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa, hivyo suala la kukamatwa kwake ndio maana hatukuliweka wazi.”
Hata hivyo, Kamanda Jongo ameongeza kuwa, “baada ya kukamilisha ukamataji wa timu nzima ambayo ilikuwa inakabiliwa na tuhuma hizo, tumeamua tuliweke wazi kwamba Imam huyu anashikiliwa na Jeshi la Polisi.”