Klabu ya Chelsea inahofia kuwa huenda watamkosa Victor Osimhen msimu wa joto, huku PSG na Arsenal zikisonga mbele katika kinyang’anyiro cha kuwania saini ya Mshambuliaji huyo wa SSC Napoli anayewindwa na klabu kibao.
Osimhen ndiye mshambuliaji anayesakwa zaidi Barani Ulaya na uhamisho wake mkubwa kutoka SSC Napoli unaelekea kutokea msimu huu wa joto, huku klabu kadhaa kubwa zikiwania saini yake.
Chelsea wamekuwa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kipindi kirefu zaidi wakiwa na kazi kubwa iliyofanywa kujaribu kumshawishi mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria kutua Stamford Bridge msimu ujao.
Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa klabu kibao za Ulaya zimekuwa katika mawindo vikisaka saini ya mchezaji huyo, ambaye hivi karibuni alikuwa na timu ya taifa ya Nigeria, ‘Super Eagles’ kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ‘Afcon 2023’ nchini Ivory Coast.
Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Didie Drogba amekuwa na mawasiliano ya karibu na Osimhen akimshawishi ajiunge na klabu hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge ili msimu ujao awe mchezaji wa klabu hiyo.
Drogba aliyestaafu kuichezea Chelsea amekuwa akizungumza na Osimhen kuhusu Chelsea na kwa nini yeye ndiye mtu kamili wa kuisaidia klabu hiyo.
Hata hivyo, PSG na Arsenal wote wanatamani huduma yake na pia wamekuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara.
Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa wababe hao wa Ufaransa wanapata imani kuwa wanaweza kumpata mshambuliaji huyo kutokana na madai yake ya mshahara.
Chelsea hawana nia ya kuwalipa wachezaji wengi kupita kiasi na kuweka muundo wao ambao umewafanya mastaa Mason Mount kusonga mbele.
Osimhen anataka angalau Pauni 200,000 (sawa na Sh milioni 650) kwa wiki na anaamini yeye ni mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani kwa sasa.
Sio PSG pekee na Arsenal pia wanawasiliana na timu ya Osimhen huku wakitathmini chaguzi za nambari tisa wanayoitaka ya kiwango cha juu.
Hilo ndilo lengo kuu la msimu wao wa kiangazi na wako tayari kunasa wachezaji kama akina Eddie Nketiah ili kuimarisha safu zao za ushambuliaji.