Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeisisitiza Serikali kutoa kipaumbele kwa Wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi na kuendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto za Wakandarasi hao ili kutoa fursa ya ushindani na Wakandarasi wa nje katika upatikanaji wa zabuni.
Hayo yameelezwa Mkoani Mwanza na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso wakati Kamati hiyo ilipokagua maendeleo ya ukarabati na ujenzi wa vivuko vinavyojengwa na Mkandarasi Mzawa Songoro Marine na kuridhishishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
“Hakikisheni mnawajali wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi kwa kuwapatia malipo kwa wakati, mkimuwezesha Mkandarasi huyu ataenda kuwekeza katika Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika na kuleta ajira kwa wananchi wa maeneo husika,” amesema Kakoso.
Kuhusu utekelezaji wa vivuko, Kamati imesema bado kuna umuhimu wa kuongeza huduma za vivuko katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mikoa ya Mara, Geita, Mwanza na Kagera hivyo Serikali ione namna ya kusimamia utekelezaji wa miradi kwa haraka ili iweze kuhudumia wananchi wa maeneo hayo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameiahidi Kamati kufuatilia malipo la Mkandarasi Mzawa Songoro Marine ili akamilishe ujenzi wa vivuko vipya vitano pamoja na ukarabati wa vivuko viwili.
“Nitahakikisha nafuatilia kwa ukaribu malipo haya Wizara ya Fedha (HAZINA), na naamini kuwa fedha zitapatikana na Mkandarasi ataendelea na utekelezaji wake kama ilivyopangwa,” amesisitiza Bashungwa.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala ameeleza kuwa Wakala huo unaendelea kusimamia ujenzi na ukarabati wa vivuko hapa nchini ,ili kuongeza utoaji wa huduma za usafiri kwa wananchi.
Akitoa taaarifa ya ujenzi wa vivuko, Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine, Khalid Songoro ameeleza kuwa katika Karakana ya Mwanza wanaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vya Kisorya – Rugezi, Ijinga – Kahangala, Bwiro – Bukondo na Nyakaliro – Kome pamoja na ukarabati wa vivuko vya Mv. Nyerere na Mv. Kilombero II.