Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amemuagiza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Rebman Ganshonga, kuhakikisha anapeleka huduma ya Maji kwenye Vitongoji ambavyo bado havina huduma hiyo.
Mhandisi Mahundi ametoa maagizo hayo akiwa katika muendelezo wa ziara ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Maji Mkoani Ruvuma na kutoa rai kwa Wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya Maji, ili miradi ya maji iwe endelevu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa usimamizi na utekelezaji wa miradi.
Amesema, “Mradi huu ukamilike kwa wakati pia wananchi muweze kutunza Miundombinu yake ili mradi uwe endelevu. Lakini chombo cha watumiaji maji katika jamii kiundwe ili kiweze kukusanya fedha na kufanya matumizi mazuri ya ukarabati wa mradi pindi inapotokea mradi umeharibika.”
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Maji Malungu, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa, Mhandisi Masoud Samila amesema mradi wa Malungu unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.2 na kwamba kukamilika kwake kunalenga kuwanufaisha wananchi wapatao 9,659 kutoka vijiji vya Malungu na Tingi vilivyopo katika kata ya Tingi.