Ni suala la muda tu lililobakia kwa Tabora United ya mjiani Tabora kutangaza uamuzi mgumu wa kuachana na kocha Goran Kopunovic kutoka Serbia kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu.
Imefahamika kuwa uongozi ulikutana na kocha na kumjulisha uamuzi wa kuachana naye na sasa umeanza mchakato wa kusaka mpya.
“Mambo mengi yamekuwa hayaendi sawa kwenye timu lakini kubwa zaidi ni muendelezo wa kufanya vibaya ambao tumekuwa nao uliopelekea tuwe katika nafasi ya hatari kwenye msimamo wa ligi.
“Kuna baadhi ya taratibu ambazo uongozi unazikamilisha kabla ya kutangaza rasmi uamuzi wa kuachana na kocha ambazo zikiwekwa sawa mambo yatakuwa hadharani,” kilifichua chanzo.
Alipotafutwa kuzungumzia taarifa hizo, Mtendaji Mkuu, Thabit Kandoro alisema Kopunovic ni kocha wa Tabora United.
Licha ya ufafanuzi huo wa Kandoro, tetesi zinaeleza kuwa mchakato wa kumsaka kocha mpya umeshaanza na ukikamilika ndipo timu hiyo itatangaza kuachana na Kopunovic.
Katika mechi 21 ilizocheza kwenye Ligi Kuu, Tabora United imepata ushindi mara nne tu, ikitoka sare tisa na kupoteza michezo saba.
Safu ya ushambuliaji inaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kumuangusha Kopunovic kwani imefunga mabao 15 ambayo imeyapata katika mechi 11 huku ikifumania nyavu katika mechi tisa tu.
Wakati ikiwa na safu dhaifu ya ushambuliaji, timu hiyo bado inahaha katika upande wa ulinzi kwani hadi sasa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 25 katika Ligi Kuu Bara.
Tabora United imebakiza mechi tisa dhidi ya JKT Tanzania, Kagera Sugar, Geita Gold, Mtibwa Sugar, Simba SC, Mashujaa, Ihefu, Young Africans na Namungo.