Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema alichagua kambi ya timu yake iwe Zanzibar kwa sababu ya wachezaji wake kupata utulivu na nafasi bora ya kufanya mazoezi kuelekea mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya Al Ahly itakayochezwa Machi 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Benchikha amesema kambi ya Zanzibar inawasaidia kufanya mazoezi asubuhi na usiku, ambao ndio muda watacheza mechi hiyo ya kimataifa na kwa kufanya hivyo wachezaji wake watazoea mazingira hayo.
Kocha huyo amesema mazoezi anayowapa ni ya kujiandaa kukabiliana na timu ngumu ya Al Ahly, mbali na mbinu za kiufundi pia anawaandaa nyota wake kuwa katika hali ya utimamu wa mwili wa hali ya juu ili kuhimili mikiki mikiki ya wamisri hao ambao wana historia nzuri katika michuano hiyo.
“Tunahitaji kufanya mazoezi mara mbili kwa siku, asubuhi na usiku ili kutengeneza timu ambayo itakwenda kutoa ushindani kwa Al Ahly, nilihitaji kufanya mazoezi muda wa usiku, muda ambao mechi yetu na Al Ahly utachezwa ili wachezaji wazoee mazingira hayo, pia huku (Zanzibar) kuna mazingira tulivu zaidi ambayo yatafanya wachezaji wetu kupumzika na akili yao kujielekeza kwenye mchezo husika,” amesema Benchika.
Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema muda wa mechi hiyo hupangwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, na si timu mwenyeji kama ambavyo wadau walitaka mchezo huo ufanyike kuanzia saa 10:00 jioni.
“Wengi walitamani mechi ipigwe mchana kwa ajili ya kuwachosha na joto, lakini mechi hizi zinapangwa na watu wengi na kwa maslahi ya wengi ikiwamo haki ya matangazo, lakini pia CAF wanaangalia ustawi wa timu zote mbili.
“Tukumbuke pia kuwa tupo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, maslahi mapana ya imani va watu wote yamezingatiwa na mechi zote zimepangwa kwenye muda huo,” amesema Ahmed