Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo 10 yanayolenga kuboresha sekta ya sheria nchini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa viwango vinavyotakiwa kiutumishi na kitaaluma.

Maagizo hayo, aliyatoa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

1. Maafisa Sheria pamoja na Mawakili wa Serikali wote nchini tekelezeni majukumu yenu ya kisheria kwa uadilifu, weledi, uwajibikaji, uaminifu, usiri, umakini na kwa kujituma. Pia, Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali nchini kote shirikianeni kikamilifu kutekeleza Kampeni ya Utoaji Msaada wa Kisheria ya Mama Samia. Hakikisheni kuwa kampeni hii inapewa uzito kama mojawapo wa majukumu yenu mahsusi.

2. Uongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na watoa huduma wengine kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inatolewa kwa wananchi wote wenye uhitaji bila ubaguzi wa namna yoyote.

3. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Taasisi nyingine za utoaji haki wafungue na kuimarisha ofisi zao katika ngazi za chini ili kuhakikisha huduma za kisheria zinafika kwa wananchi wote kwa wakati na bila usumbufu.

4. TAMISEMI iratibu Kamati za Mikoa za Kuratibu Huduma za Msaada wa Kisheria ambazo nyingi kwa sasa hazifanyi kazi, ziwezeshwe kifedha na kupewa nyenzo ili ziweze kuwahudumia wananchi katika mikoa yao kwa tija na wepesi.

5. Wizara ya Katiba na Sheria ishirikiane na Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuweka mipango ya kutafuta vyanzo vya fedha ili kuwezesha kamati za mikoa kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kushirikiana na wadau wake wa sheria, ihakikishe watoa huduma wote, bila kujalisha maeneo walipo, wanawezeshwa fedha na nyenzo za kazi na kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili yawasaidie kutekeleza majukumu yao.

6. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iwezeshe upatikanaji wa nakala za miongozo iliyotokana na sheria zote zilizofanyiwa urekebu na ufasiri ili kusaidia watoa huduma za msaada wa kisheria.

7. Wananchi wazielewe na kuzitumia. Wananchi watumie fursa ya uwepo wa tafsiri za sheria kwa lugha ya Kiswahili ili kufahamu haki zao. Ninawapongeza sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi ya ufasiri wa sheria za nchi kwa Kiswahili.

8. Mawakili wote wa Serikali wajisajili kwenye mfumo wa OAG-MIS. Hii itawawezesha wananchi kuwajua mahali mlipo na kurahisisha upatikanaji wa huduma za sheria mbalimbali.

9. Mahitaji makubwa ya wananchi yanahusiana na upatikanaji wa elimu katika utatuzi wa migogoro kwenye makosa ya jinai, ndoa, ardhi, kazi na mirathi. Hivyo basi, wekeni mkakati mahsusi wa kuendelea kuelimisha wananchi katika maeneo hayo.

10. Serikali itaendelea kutoa rasilimali muhimu ili kuziwezesha taasisi hizo zitoe huduma kwa ufanisi. “Kundi hili kubwa la Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali limebeba dhamana kubwa ya kutoa huduma za kisheria. “nendeni mkaitendee haki dhamana hii kubwa kwa ustawi wa wananchi wa Tanzania,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Leseni 2,648 za Madini zafutwa, onyo kali latolewa
Benchikha achekelea kambi Zanzibar