Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Mecky Maxime amesenma kusimama kwa ligi kunapunguza ari ya upambanaji wa timu yake katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha huyo amesema wamekuwa na kiwango bora tangu kuanza kwa mzunguko wa pili jambo ambalo limewasaidia kupata matokeo chanya na kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo lakini ghafla ligi imesimama.
“Nafahamu ni kalenda ya FIFA lakini hii wakati mwingine huwa inatuharibia ligi itakapoendelea itatulazimu kucheza mechi tatu hadi nne ili kurudi kwenye kiwango chetu tulichokuwa nacho kabla ligi kusimama,” amesema Maxime.
Kocha huyo amesema ili kuepuka hilo atajitahidi wapate mechi nyingi za kirafiki kitu ambacho si rahisi sana kwa sababu timu nyingi hasa za ligi ya Championship zipo kwenye mapambano ya kumaliza msimu.
Amesema utaratibu huo unaziumiza timu ambazo hazina wachezaji kwenye timu za taifa kwani kwa kipindi chote cha wiki mbili ambacho ligi imesimama timu hizo zinaishia kufanya mazoezi ya wenyewe kwa wenyewe.
Ihefu FC ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo ikikusanya alama 23 katika michezo 21 iliyocheza na imebakiwa na michezo tisa kumaliza msimu.