Miamba ya soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich imeripotiwa kuwa na mpango wa kumchagua Antonio Conte kuwa kocha wao mpya, imeelezwa.

Kocha huyo kutoka nchini Italia amekuwa hana kazi tangu Machi mwaka jana alipofutwa kazi Tottenham.

Lakini, anaweza kushawishika na nafasi hiyo ya kwenda kufanya kazi Ujerumani kwa mara ya kwanza kutokana na Bayern Munich kudaiwa kuhitaji huduma yake.

Na hilo litampa nafasi ya kwenda kufanya kazi na Mshambuliaji Harry Kane kwa mara nyingine baada ya awali kuwa pamoja kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur.

Conte anatazamwa na Bayern kama mtu muhinu kwenda kuchukua mikoba ya kocha Thomas Tuchel, ambaye ataachana na miamba hiyo ya Allianz Arena mwishoni mwa msimu huu 2023/24.

Shida ipo kwenye kufikia makubaliano, ambapo Conte atahitaji mshahara mkubwa baada ya kuvuna Pauni 15 milioni kwa mwaka alipokuwa Spurs.

Bayern ina majina ya makocha kadhaa inayowafikiria kuwapa kazi, akiwamo wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso.

Conte mwenye umri wa miaka 54, alishinda taji la Ligi Kuu England na Serie A mara nne katika klabu mbili tofauti.

Aliwezesha pia Spurs kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumfanya Kane kucheza soka la kiwango cha juu sana, ambapo alifunga mabao 32 chini ya kocha huyo msimu uliopita.

Mexime achukizwa ligi kusimama
Che Fondoh Malone: Zanzibar itatusaidia sana