Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini – TUCTA, limesema litaanza kutoa rasmi Gazeti maalum litakalozungumzia masuala mbalimbali ya Wafanyakazi ambalo litaitwa Mfanyakazi Tanzania.

Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya akiongea mbele ya Waandishi wa Habari amesema, Gazeti hilo linamilikiwa na shirikisho na linasimamiwa na Kampuni Tanzu ya ‘Workers Development Corporation’ – WDC.

Amesema, Gazeti hilo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa 2024, jijini Arusha.

“Kwa kipindi cha nyuma TUCTA ilikuwa na chombo chake cha habari ambacho ni gazeti lililokuwa maarufu na lilikuwa likiitwa Mafanyakazi. Hiki ndicho chombo cha habari kilichokuwa kinatumika na Vyama vya Wafanyakazi katika kutoa habari kwa wafanyakazi na umma kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, uchumi, siasa, kimataifa, burudani na michezo,” alisema.

Nyamhokya ameongeza kuwa, Gazeti hilo lilikuwa likitoka mara mbili kwa juma kwa siku za Jumatano na Jumamosi, lakini kutokana na changamoto za kiundeshaji likawa linatoka mara moja kwa wiki na kuanzia mwaka 2012 likashindwa kuendelea kutokana na sababu mbalimbali.

Amesema, “TUCTA kupitia vikao vyake vya kikatiba imetafakari upya umuhimu wa kufufua gazeti lake la mfanyakazi na hivyo mchakato ulifanyika na tumefanikiwa kupata usajili kutoka Idara ya Habari – Maelezo Machi 27, 2024 ambapo kwa sasa gazeti hilo litajulikana kwa jina la Mfanyakazi Tanzania.”

Kagera: Wanawake zaidi ya 400 wakutwa na maambukizi ya Saratani
Alaji ya Lori kusombwa na maji: Miili mitano yaopolewa