Wakati mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya Young Africans na Mamelodi Sundowns unakaribia kuchezwa, huko Mamelodi kimenuka.

Ni hivi, kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Hugo Broos amesema amechukizwa na kitendo cha Kocha wa Mamelodi, Rhulani Mokwena kutangaza wachezaji saba wa timu hiyo ni majeruhi hivyo hawatojiunga na timu ya taifa, badala ya kufuata taratibu zinazotakiwa.

Taarifa nyingine zinaeleza Mamelodi inakwepa kuwaachia mastaa hao kwa sababu wapo kwenye maandalizi ya mechi yao dhidi ya Young Africans, hivyo wanahofia ikiwa watawaachia watapata muda mchache wa kujiandaa na huenda wakapata majeraha zaidi.

Mamelodi itacheza ugenini kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam Machi 30 dhidi ya Young Africans katika mechi ya mkondo wa kwanza wa kuwania kufuzu Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana siku sita baadae huko Afrika Kusini.

Katika mechi ya mwisho kabla ya juma la mapumziko kwa ajili ya kupisha kalenda ya kimataifa wa FIFA, Sundowns ilicheza dhidi ya Maritzburg United kwenye mchezo wa Nedbank Cup hatua ya 16 bora, huku ikiwa haina wachezaji wake muhimu saba.

Mastaa hao saba ni pamoja na Ronwen Williams, Teboho Mokoena, Themba Zwane ambao wameumia hivi karibuni wakiungana na Thapelo Maseko Mothobi Mvala na Khuliso Mudau waliopo nje tangu waliporudi kutoka kwenye fainali za Mataifa va Afrika ‘AFCON 2023’ na Bafana Bafana ilimaliza nafasi ya tatu.

Licha ya kutokuwepo kwenye mechi hiyo ya Nedbank Cup, kipa Willianms, Mokoena na Zwane wote walijumuishwa kwenye kikosi cha Afrika Kusini kinachotarajiwa mechi mbili za kirafiki dhidi ya Andorra na Algeria.

Baada ya kujumuishwa kwenye kikosi, Kocha Mokwena alisema kipa wake Williams bado anatibiwa bega wakati Mokoena akisumbuliwa na tatizo la goti.

Siku kadhaa baada ya Mokwena kusema hivyo, Broos akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema Mokwena hajafikisha taarifa hizo kupitia njia sahihi, hivyo yeye anachofahamu wachezaji aliowaita wote ni wazima na anawahitaji kambini.

“Kama wachezaji kweli wameumia, walitakiwa watuambie ma sio kuongea kwenye vyombo vya habari, tuna daktari na wao wanafahamu sisi tuna daktari na wana namba yake ya simu, kwa nini wasimpigie na kumpa hizo taarifa.

“Hawakufanya hivyo ikiwa na maana wachezaji wote ni wazima, samahani sana siwezi kufanya kazi kwa maneno yaliyosemwa na kocha Rhulani, labda Mkurugenzi wa Ufundi aniambie ni kweli wanaumwa. Tofauti na hivyo, wampe ripoti daktari wa timu yeye ndio ataamua wanaumwa kweli au laah.”

Taharuki Kilosa: Ulinzi na usalama wafika eneo la tukio
Undani sakata la ufutaji Leseni 2,648 sekta ya Madini