Umoja wa Mashabiki wa klabu ya Chelsea wameandika barua kwenda kwa wamiliki wa klabu hiyo, Todd Boehly na Behdad Eghbali wakisema timu hiyo imekuwa kichekesho ndani na nje ya uwanja.
Barua hiyo ililaumu uongozi wa klabu hiyo na kuainisha mambo mbalimbali yanayowagusa mashabiki wa klabu hiyo tangu mwaka 1980.
Todd Boehly na kampuni ya Clearlake Capital waliinunua Chelsea Mei 2022 na wametumia zaidi ya Pauni Bilioni 1 kwenye usajili wa wachezaji.
“Malengo yetu kama wamiliki yako wazi. Tunataka kuwafanya mashabiki wajivunie klabu hii,” alisema Boehly kwenye taarifa yake wakati mpango wa kuinunua klabu hiyo ulipothibitishwa.
Ingawa, barua kutoka kwa Umoja wa Mashabiki wa klabu hiyo inaonesha kwamba bado hawajaridhishwa na namna inavyoendeshwa.
“Umoja wa Mashabiki wa Chelsea unasikitika kuamini kwamba tunakaribia kama sio tayari tunashuhudia kupuuzwa kwa maoni ya mashabiki yanayoweza kubadili matokeo ya timu uwanjani,” ilisema barua hiyo.
“Kama hali haitabadilika, inaweza kusababisha mashabiki kuzomea, hasa kwenye mechi zinazooneshwa kwenye televisheni na baadhi ya mashabiki kujipanga kuandamana kupinga.
Umoja huo pia ulisema kukosekana kwa mawasiliano kwenye mambo mbalimbali unawachanganya mashabiki wa klabu hiyo.
“Hali ya furaha kwa sasa miongoni mwa mashabiki imeshuka sana na haiwezi kupuuzwa.
“Hisia ni kwamba klabu imekuwa kichekesho ndani na nje ya uwanja,” iliongeza barua hiyo.
“Mashabiki wanasema kwamba kwa sasa inaonekana kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na imani na uongozi wa klabu hiyo, hasa kundi linaloenda uwanjani kutokana na kupungua kwa mawasiliano. Mashabiki wengi wanahofu kuhusu hatima ya muda mfupi na mrefu kwenye klabu yetu.”