Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimetakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa nchi zao zinakuwa na amani, Umoja na utulivu na kutafuta ufumbuzi wa migogoro kwa kutumia njia zao wenyewe.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mulambo Haimbe wakati anafungua Mkutano huo uliofanyika jijini Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.
Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo baada ya Zambia na inawakilishwa katika Mkutano huo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine unapokea ripoti ya utekelezaji wa vikosi vya kulinda amani katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na mchakato unaoendelea wa kupeleka vikosi vya kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Nchi Wanachama zimehimizwa kuimarisha zaidi mshikamano na kuchangia rasilimali walizonazo ili kuviangamiza vikundi vya waasi vinavyotishia amani kwenye Kanda ya SADC. Imeelezwa kuwa bila ya amani na Usalama katika Kanda hiyo, wananchi wasitarajie kufikiwa kwa mtangamano na maendeleo ya kweli.
Mkutano huo wa Mawaziri ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC utakaofanyika Machi 23, 2024 ambapo Tanzania itawakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango.