Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, linamshikilia Mohamed Omary Salahange (37), mkazi wa Rudewa Gongoni Wilayani Kilosa kwa tuhuma za kumuua kisha kumzika kwenye chumba walichokuwa wakiishi, mke wake Beatrice Talius Ngongolwa.

Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro SACP, Alex  Mkama amesema jeshi hilo lilipokea taarifa za siri kuhusu mauaji hayo Machi 21, 2024 zilizoeleza kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo alitenda kosa hilo na kuhama kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na mkewe.

Amesema, baada ya kukamatwa na kuhojiwa mtuhumiwa alikiri kufanya mauaji hayo na aliwapeleka maafisa wa polisi kwenye eneo la tukio ambako jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali pamoja na kamati ya usalama Wilaya ya Kilosa, kisha waliufukua mwili wa mwanamke huyo kwa ajili ya uchunguzi.

Akizungumza tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa baada ya kufanya mahojiano na watoto wa mama huyo (Beatrice Haiyasi), walieleza jinsi walivyopitia unyanyasaji mpaka kupelekea kukosa huduma muhimu za kielimu, kutokana na kufungiwa ndani.

“Tulipata taarifa za mama huyu kuuawa na mume wake kutoka kwa wasamaria wema hii ni baada ya kutokea ugomvi kati ya mtuhumiwa na mke wake wa sasa ndipo watoto wa marehemu wakaanza kumkanya mama huyo kuwa asigombane na mtuhumiwa huyo kwani atauawa kama alivyouawa mama yao ndipo mama huyo akatoa taarifa kwa mamlaka husika,” alisema Shaka.

 

Vifo zaidi ya watu 400: Ripoti ya Shakahola ilipuuzwa
SADC: Bila amani hakuna mtangamano, maendeleo