Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutoa misaada ya kibinadamu na urejeshaji wa hali kutokana na athari zilizosababishwa na Kimbuga HIDAYA kwenye maeneo ya Kilwa, Mafia, Rufiji na Ifakara.

Majaliwa ameyasema hayo wakati akitoa taarifa rasmi kuhusu kimbunga Hidaya kilichotokea Mei 3, 2024 katika Pwani ya Bahari ya Hindi, na kudai kuwa hatua hizo za Serikali zimeshirikisha Wizara za Kisekta, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi mbalimbali pamoja na wadau wengine muhimu.

Amesema, hatua zilizochukuliwa katika Wilaya ya Kilwa ni pamoja kuendesha zoezi la utafutaji na uokokoaji ambapo jumla watu 4,080 wameokolewa katika maeneo mbalimbali.

“Hatua nyingine ni kurejesha hali ya miundombinu ya barabara kuu ya Lindi – Dar es Salaam. TANROADS wapo eneo la tukio wanaendelea na kazi; Juhudi zinafanyika za urejeshaji wa daraja la Somanga – Mtama ili magari yaliyokwama yaendelee na safari.”

Waziri Mkuu amesema hatua zilizochukuliwa katika Wilaya za Rufiji na Kibiti ni pamoja na Kutoa huduma ya Afya ya Akili, Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii kwa waathirika 1,941 (1,501 Kibiti na 440 Rufiji), Kuwaunganisha waathirika 24 (12 Rufiji na 12 Kibiti) walio kambini na huduma za matibabu na hivyo kufanya idadi ya waathirika waliofikiwa na huduma hiyo hadi sasa kufikia 912 (472 Kibiti na 440 Rufiji) na Kutoa elimu ya usafi, ulinzi na usalama kwa mtoto kwa waathirika 1,023 (583 Kibiti na 440 Rufiji).

Katika Wilaya ya Mafia, Waziri Mkuu amesema hatua zilizochukuliwa ni kuwaunganisha waathirika na ndugu na majirani ili wapate hifadhi ya muda baada ya nyumba zao kubomoka na kuzingirwa na maji. Kwa upande wa Kilwa Waziri Mkuu amesema Serikali imeanzisha makazi ya muda kwenye shule za Msingi ambapo kwa sasa wananchi wapo kwenye vituo vitatu vya Shule za Msingi za Mchakama, Ruhatwe na Ndende.

Jaribio la kumuuwa Zelensky laondoka na Mkuu wa Usalama
Zaidi ya 49 wapatiwa huduma za kibingwa Tanganyika