Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema bado anapambana kuhakikisha Klabu hiyo inafikia malengo waliyojiwekea msimu huu, licha ya kikosi chake kutopewa nafasi ya kutwaa Ubingwa.

Simba SC imeendelea kuwa nafasi ya tatu, licha ya kushinda mchezo wake wa jana Alhamis (Mei 09) dhidi ya Azam FC iliyokubali kufungwa 3-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikizidiwa alama moja na wababe hao wa Chamazi, huku Young Africans ikiwa kileleni kwa kufikisha alama 68.

Mgunda amesema pamoja na wadau wengi wa Soka la Tanzania kuamini Simba SC haina nafasi ya kuwa mabingwa msimu huu, lakini anachofahamu Michuano ya Ligi ni kama Marathon, hivyo wanatakiwa kusubiri hadi mwisho wa msimu ndipo waamue.

“Haya ni mshindano, na mara nyingi Ligi ni kama mbio za Marathon, kuna anayeongoza na mwingine anayemfuatia lakini mwisho wa siku yule atakayekata utepe mwisho ndio atakuwa mshindi ama bingwa, kwa hiyo sisi tunajipanga na michezo iliyo mbele yetu kuhakikisha tunafanya vizuri alafu mwisho wa yote tutaangali tumesimama wapi na tumepata kitu gani.” amesema Mgunda

Ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam FC umeiwezesha Simba SC kufikisha alama 56 ikitanguliwa na Wanalambalamba hao kutoka Chamazi jijini Dar es salaam, wanaoshika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 57.

Ikumbukwe kuwa Bingwa wa Tanzania Bara na Mshindi wa Pili watapata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Mshindi watatu na Bingwa wa Kombe la Shirikisho (CRDBFC) watashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao 2024/25.

Siri za Balua, Chasambi zafichuliwa
Ahmed Ally: Mgunda anastahili kupewa Simba SC